Netanyahu aionya Iran katika mkutano wa usalama Munich
18 Februari 2018Akishikilia kipande cha kile alichosema kuwa ni ndege ya Iran isiyokuwa na rubani baada ya kuingia katika anga ya Israel mapema mwezi huu, Netanyahu ameuambia mkutano wa usalama mjini Munich, kwamba "Israel haitauruhusu utawala huo kuweka kitanzi cha ugaidi katika shingo.
"Tunachukua hatua iwapo itakuwa muhimu sio tu dhidi ya washirika wa Iran lakini dhidi ya Iran yenyewe ," alisema.
Akiuhutubia mkutano wa usalama mjini Munich kwa mara ya kwanza, Netanyahu amewataka maafisa wa Marekani na Ulaya waliokusanyika pamoja na wanadiplomasia kupambana na Iran haraka, akionesha ramani inayoonesha kile alichosema kuwa ni uwepo wa Iran unaoongezeka katika mashariki ya kati.
Amesema Iran inaongeza nguvu zake wakati muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria unakomboa maeneo kutoka kwa wanamgambo hao.
Himaya ya Iran
"Kitu cha kusikitisha ni kwamba wakati IS inapotea na Iran inachukua maeneo yake, inajaribu kujenga himaya inayoendelea ikizunguka eneo la mashariki ya kati kutoka kusini nchini Yemen lakini pia ikijaribu kujenga daraja la ardhini kutoka Iran kwenda Iraq , Syria , Lebanon na Gaza," Netanyahu alisema. "Hizi ni hatua za hatari kwa eneo letu."
Wasiwasi uliongezeka mnamo Februari 10 wakati kombora la kupambana na ndege za kivita lilipoiangusha ndege ya kivita ya Israel ikirejea kutoka kufanya mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na Iran nchini Syria. Hayo ni mapambano halisi hadi sasa kufanywa na Israel na majeshi yanayoungwa mkono na Iran yaliyoko katika mpaka.
Wakati huo huo msemaji wa waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, ameamua kutotilia maanani maneno ya waziri mkuu yanayobadilisha mtazamo wa Poland wa ushirika katika mauaji ya Wayahudi , Holocaust na kuwa ni madai ya "Wayahudi wakosaji" kwa kusema ni matamshi ya kukaribisha mjadala wa wazi juu ya uhalifu wa vita vikuu vya pili vya dunia dhidi ya Wayahudi.
Wanasiasa wa Israel wamemshutumu waziri mkuu wa Poland kwa chuki dhidi ya Wayahudi kufuatia matamshi yake hayo jana Jumamosi (17.02.2018) katika mkutano wa usalama mjini Munich, akifungua ukurasa mpya katika mzozo wa hasira kuhusiana na sheria mpya ya Poland inayopita marufuku baadhi ya hotuba za mauaji ya Holocaust.
Msemaji wa Morawiecki Joanna Kopcinska amesema leo Jumapili kwamba maneno yake "yanapaswa kutafsiriwa kama wito wa moyo mkunjufu kwa ajili ya majadiliano ya uhalifu uliotendeka dhidi ya Wayahudi wakati wa mauaji ya Holocaust, bila kujadili utaifa wa wale waliohusika. Taarifa hiyo iliyotolewa kwa lugha ya Kipolish na Kiingereza imesema matamshi ya Morawiecki " kwa vyovyote vile hayakulenga kukana kuhusu Holocaust."
Mwandishi: Sekione Kitojo /rtre / ape
Mhariri: Lilian Mtono