1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Netanyahu aishutumu Marekani kwa kuzuia msaada wa silaha

19 Juni 2024

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amedai kwamba Marekani imekuwa ikizuia silaha inazozihitaji kwa ajili ya vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameishutumu Israel kwamba inazuia silaha inazozihitaji kwenye vita dhidi ya HamasPicha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Kwenye taarifa ya vidio iliyochapishwa Jumanne Netanyahu alisema hatua hiyo ilikuwa inapunguza kasi ya mashambulizi yake katika mji wa Rafah ulioko Kusini mwa Gaza.

Amesema hayo, wakati Umoja wa Mataifa ukiishutumu Israel kwa kukiuka mara kwa mara sheria za kimataifa kwenye vita hivyo baada ya kushindwa kutofautisha wapiganaji na raia. 

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema jana kwamba ni wazi kwamba katika kipindi cha miezi michache iliyopita, serikali ya Marekani imekuwa ikizuia silaha na risasi kwa ajili ya Israel.

"Wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alipokuwa hapa hivi karibuni tulizungumza kwa uwazi. Nilisema ninathamini sana msaada ambao Marekani imewapa Israel tangu mwanzo wa vita. Lakini nilisema na kitu kingine, nilisema ni dhahiri kwamba katika miezi michache iliyopita Marekani ilikuwa ikizuia silaha kwa ajili ya Israel,"

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu(kulia) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, alipofanya ziara hivi karibuni nchini Israel.Picha: Amos Ben-Gershom/GPO/dpa/picture alliance

Rais Joe Biden alichelewesha upelekwaji wa baadhi ya silaha nzito nchini Israel tangu mwezi Mei kutokana na mashaka kuhusiana na mauaji ya raia katika Ukanda wa Gaza. Alikiri kwamba raia walikuwa wanauliwa na aina ya mabomu makubwa ambayo Marekani imekuwa ikiyapeleka Israel.

Soma pia: Wizara ya Afya Gaza yasema vifo vya vita vimefikia 37,296

Hata hivyo, Blinken alisema siku ya Jumanne kwamba mabomu hayo ya tani 2,000 ndio silaha pekee zinazofanyiwa ukaguzi.

Blinken hata hivyo, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kila kitu kinaendelea kama kilivyopangwa katikati ya ongezeko la ukosoaji wa kimataifa wa msaada huo wa Marekani kwenye vita hivyo vilivyofikia mwezi wa tisa kwenye eneo hilo la Palestina.

Mtoto wa Kipalestina akitembea mbele ya nyumba iliyoharibiwa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Mjini Geneva, Umoja wa Mataifa umesema hii leo kwamba vikosi vya Israel huenda vikawa vimekiuka mara kadhaa misingi mikuu ya sheria za kivita na kushindwa kutofautisha kati ya wapiganaji na raia katika operesheni hiyo ya kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza.

Kwenye ripoti inayochunguza mashambulizi sita ya Israel yaliyosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, vifo na majeruhi, Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja huo Volker Turk amesema, Israel huenda ilinuia kukiuka kanuni za kutofautisha, uwiano na tahadhari katika mashambulizi.

Zaidi ya watu 37,369 wamekufa hadi sasa hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.

Huko Ukanda wa Gaza kwenyewe, mashambulizi ya anga na mapigano kati ya Israel na Hamas yameitikisa Gaza hii leo, huku jeshi la Israel likitahadharisha kwamba limejiandaa na "mashambulizi" dhidi ya harakati za wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon kwenye mpaka wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW