1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu akabiliwa na shinikizo la kuidhinisha makubaliano

17 Januari 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa maafisa wa serikali yake wameafikiana kuhusu mpango wa kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka licha ya mivutano iliyoshuhudiwa dakika za mwisho.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Pool European Pressphoto Agency/AP/dpa/picture alliance

Netanyahu amesema hivi punde kuwa maafisa wa Israel hatimaye wameafikiana kuhusu makubaliano ya kuwarejesha mateka licha ya mivutano iliyoshuhudiwa. Siku ya Alhamisi, Netanyahu aliituhumu Hamas kuwa inajaribu kuzuia mpango huo, tuhuma ambazo zilikanushwa vikali na  kundi hilo. Hata hivyo, mkutano wa leo Ijumaa wa Baraza la Mawaziri ndio unatarajia kuidhinisha au la mpango huo wa usitishwaji mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

Awali, Netanyahu alikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia ambao ni washirika wake kwenye serikali na wanaopinga kabisa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka.

Soma pia: Israel yasogeza mbele muda wa kuidhinisha makubaliano, yaishutumu Hamas kwa ukiukwaji

Waziri wa Fedha mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Bezalel Smotrich alisema mpango wa kusitisha mapigano Gaza unahatarisha zaidi usalama wa Israel na itakuwa ni ishara ya kusalimu amri mbele ya Hamas.

Kwa upande wake waziri wa usalama wa Israel kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben Gvir alisema Alhamisi jioni kwamba yeye na wanachama wenzake watajiondoa katika baraza la mawaziri iwapo litaidhinisha makubaliano hayo, na kwamba atarejea serikali ikiwa tu  vita dhidi ya Hamas vitaendelea ili kufanikisha malengo ambayo amesema hadi sasa hayajafikiwa.

Mara kadhaa viongozi hao wawili wamekuwa wakipinga kabisa hatua zozote za usitishwaji mapigano wakisema kuwa ili kufanikisha zoezi la kuachiliwa kwa mateka, ni lazima kusitisha misaada yote ya kibinadamu inayotumwa Gaza ili kuishinikiza Hamas kusalimu amri.

Misri yashinikiza kutekelezwa kwa mpango huo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr AbdelattyPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty amezitolea wito Israel na Hamas kutekeleza mara moja makubaliano hayo ya usitishaji mapigano Gaza na hivyo kuongeza shinikizo kwa Netanyahu ili kuidhinisha mpango huo unaotakiwa kuanza kutekelezwa rasmi Jumapili mchana.

Soma pia: Baraza la Israel kupiga kura kuhusu kusitisha mapigano Gaza

Baraza la mawaziri la Israel linatarajiwa leo Ijumaa kuamua ikiwa linaidhinisha au la makubaliano hayo, huku Marekani  ikitaja kuwa na imani kuwa mpango huo utaanza kutekelezwa kama ilivyopangwa.

Hayo yakiarifiwa, mashambulizi mapya ya Israel yamesababisha vifo vya makumi ya watu huko Gaza huku jeshi la Israel likisema kuwa lilishambulia takriban maeneo 50 katika ukanda huo.

(Vyanzo: DPA, AP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW