1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aapa kupinga kuanzisha taifa la Palestina

17 Novemba 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kupinga jaribio la kuanzisha taifa la Palestina, siku moja kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura kuhusu azimio lililoandaliwa na Marekani kuhusu Gaza.

Israeli Jerusalemu 2023 | Benjamin Netanyahu katika mkutano na waandishi wa habari
Benjamin Netanyahu katika mkutano na waandishi wa habariPicha: Ronen Zvulun/UPI Photo/IMAGO

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kupinga jaribio lolote la kuanzisha taifa la Palestina, siku moja kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura kuhusu azimio lililoandaliwa na Marekani kuhusu Gaza, ambalo linaacha mlango wazi katika uwezekano wa uhuru wa Palestina. Netanyahu pia alikataa marejeleo yoyote katika pendekezo la Marekani kuhusu kuondoa silaha Gaza. Katika taarifa yake hiyo ya Jumapili kwa baraza lake la mawaziri alibainisha kuwa pendekezo hilo linataka Gaza iwe bila silaha na Hamas ipokonywe silaha. Kimsingi Baraza la Usalama linatarajiwa kupiga kura kuhusu pendekezo la Marekani la kutoa mamlaka ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuanzisha kikosi cha kimataifa cha kudumisha utulivu Gaza, licha ya upinzani kutoka Urusi, China na baadhi ya nchi za Kiarabu.