1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu anaelekea kushinda Israel

10 Aprili 2019

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anaonekana kushinda katika uchaguzi wa nchi hiyo hatua inayomuweka katika nafasi ya kuunda serikali ya muungano na kuurefusha muhula wake madarakani.

Israel Wahlen Wahlparty Netanjahu
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Schalit

Huku asilimia 97.4 ya kura zikiwa zimeshahesabiwa, matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jana Jumanne yanaonesha kuwa chama cha Likud cha Netanyahu na washirika wake wa kisiasa kimepata ushindi wa viti 65 katika bunge la Israel lenye viti 120 na bila shaka chama hicho kitakuwa kwenye nafasi ya kuunda serikali ijayo ya muungano ya mrengo wa kulia.

Hii itakuwa mara ya tano kwa Netanyahu kuiongoza Israel na hatua hiyo inamuweka katika nafasi ya kuwa waziri mkuu aliyeiongoza Israel kwa muda mrefu zaidi baadae mwaka huu na kumshinda David Ben-Gurion muasisi wa taifa hilo.

Likud na Blue and White zafungana

Chama cha Likud kinaonekana kupata idadi sawa ya viti bungeni na chama hasimu cha Blue and White muungano unaofuata siasa za wastani ambao unaongozwa na aliyekuwa mkuu wa majeshi, Benny Gantz. Netanyahu na Gantz wote wamedai kushinda katika uchaguzi huo. Waziri Mkuu Netanyahu amesema amefurahishwa na ushindi huo mkubwa na kwamba tayari ameanza kuzungumza na washirika wake watakaounda serikali ya muungano.

Kiongozi wa muungano wa Blue and White, Benny GantzPicha: Reuters/A. Cohen

''Nimeguswa sana na hatua ya taifa la Israel kwa mara nyingine tena kuniamini kwa muhula watano, hiyo ni imani kubwa zaidi. Ninawahakikishia kuwa ninakusudia kuikamilisha kazi hii haraka iwezekanavyo. Hii itakuwa serikali ya mrengo wa kulia, lakini mimi nitakuwa waziri mkuu wa raia wote wa Israel,'' alisema Netanyahu.

Maoni ya Gantz

Kwa upande wake Gantz amesema leo asubuhi ushindi wake utakuwa kwa ajili ya kila mmoja na kwamba atakuwa waziri mkuu wa kila mtu. Kuchaguliwa tena kwa Netanyahu, mwenye umri wa miaka 69, kutamuimarisha kiongozi huyo anayekabiliwa na makosa ya jinai katika mlolongo wa kashfa za rushwa.

Matokeo yaliyotangazwa leo hayajazijumuisha kura za maaskari, wafungwa na wanadiplomasia. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa kesho mchana hatua inayoweza kubadilisha idadi ya asilimia za kura.

Washirika wawili muhimu wa Netanyahu, waziri wa zamani wa ulinzi, Avigdor Lieberman na Waziri wa Fedha, Moshe Kahlon bado hawajathibitisha rasmi kama wataungana na Netanyahu.

Kwa vyovyote vile Israel inakabiliwa na kile kinachoonekana kuwa wiki kadhaa za mazungumzo ya kisiasa kuhusu muundo wa muungano utakaotawala. Bunge jipya litaapishwa Aprili 23 na serikali mpya inatarajiwa kuapishwa ifikapo mwanzoni mwa mwezi Juni.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW