Netanyahu aomba kupatiwa msamaha wa Rais
30 Novemba 2025
Netanyahu, ambaye amekuwa akipambana na mfumo wa sheria wa nchi hiyo kutokana na mashtaka yanayomkabili, amesema ombi lake lina lengo la kuiunganisha tena nchi hiyo hasa katika wakati wa mabadiliko makubwa kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.
Hata hivyo ombi hilo tayari limezusha ukosoaji mkali kutoka kwa wapinzani wake, ambao wamesema iwapo litakubaliwa litautia doa mfumo wa utoaji haki na taasisi za kidemokrasia na kuonesha kana kwamba Netanyahu yuko juu ya utawala wa sheria,
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumapili, Ofisi ya Waziri Mkuu huyo imesema Netanyahu amewasilisha ombi rasmi la kupatiwa msamaha kwenye ofisi ya sheria ya rais wa nchi hiyo.
Ofisi ya rais imekiri kupokea ombi ikilitaja kuwa lenye uzito mkubwa na kwamba matokeo yake yatakuwa na umuhimu kwa mustakabali wa Israel. Mwenyewe Netanyahu amesema analenga kufikisha mwisho kesi dhidi yake ambayo imesababisha mgawanyiko mkubwa kwenye taifa hilo.
Kesi ya "kumsaka mchawi" imeliwaga taifa: Netanyahu
Netanyahu amekuwa waziri mkuu wa kwanza aliye madarakani kusimama kizimbani katika historia ya Israel.
Anatuhumiwa kwa ulaghai, kuvunja kiapo cha utumishi na kupokea rushwa katika kesi tatu tofauti zinazomtuhumu kutoa upendeleo kwa wafuasi wake matajiri.
Hadi sasa bado hajatiwa hatiani kwa makosa yoyote yanayomkabili.
Mwenyewe anakunusha madai dhidi yake na amelaani kesi hizo akizitaja kuwa "mashtaka ya kumsaka mchawi" yaliyopaliliwa na vyombo vya habari, polisi na mahakama.
Ombi la Netanyahu limewasilishwa wiki kadhaa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kumrai rais Isaac Herzog kumsamehe waziri mkuu huyo.
Mapema mwezi huu, Trump pia alituma barua kwa Rais Herzog akiitaja kesi ya Netanyahu kuwa "mashtaka yaliyochochewa kisiasa na yasiyo na msingi."
Katika ujumbe wa video, Netanyahu amesema kesi dhidi yake imeligawa taifa na kwamba msamaha utarejesha umoja ndani ya Israel.
Pia amesema sharti la kumtaka kufika mahakamani mara tatu kila wiki limekuwa changamoto kubwa kwa upande wake kuiongoza vizuri serikali.
"Kuendelea kwa kesi hii kunatusambaratisha sisi wenyewe, kunaongeza migawanyiko na kuzidisha tofauti baina yetu, Nina hakika, kama ilivyo kwa wengine humu nchini, kwamba kuhimitishwa haraka kwa keshi hii kutasaidia sana kupunguza joto na kuharakisha maridhiano ambayo taifa letu linayahitaji sana, " amesema Netanyahu.
Netanyahu amesimama kizimbani mara kadhaa mwaka uliopita, lakini kesi yake imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kumruhusu kushughulikia vita na machafuko yaliyotokana na shambulizi la Hamas la Oktoba 2023.
Upinzani na wanaharakati wapinga ombi la Netanyahu
Ombi la msamaha la Netanyahu linajumuisha nyaraka mbili -- moja ni barua iliyotiwa saini na wakili wake na nyingine ni barua aloitia saini mwenyewe.
Zitapelekwa kwanza kwenye wizara ya sheria ya nchi hiyo ili kupata tathmini ya kisheria na kisha zitawasilishwa kwa mshauri wa sheria kwenye ofisi ya Rais ambayo itaandaa mapendekezo na ushauri zaidi kwa Rais,
Wataalamu wa sheria wamesema ombi la msamaha haliwezi kuzuia kuendelea kwa kesi.
"Haiwezekani," amesema Emi Palmor, katibu mkuu wa zamani wa wizara ya sheria alipozungumza na shirika la habari la Associated Press.
"Huwezi kusema kwamba huna hatia wakati kesi inaendelea na unakuja kwa rais kumwomba aingilie kati," amesema. Njia pekee ya kusimamishwa kesi hiyo kwa mujibu wa Palmor ni kwa mwanasheria mkuu wa serikali kutangaza kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.
Ombi la msamaha la Netanyahu limezusha ukosoaji mkali kutoka kwa wapinzani na makundi ya kupigania demokrasia ambayo yamemtolea mwito rais Herzog kutokubali ombi hilo.
"Hauwezi kumpatia mtu msamaha kabla ya kukiri kosa, kuonesha majuto na kutangaza kujitoa mara moja kwenye maisha ya siasa," amesema kiongozi wa upinzani Yair Lapid.