Netanyahu aonyesha mshikamano na wananchi wa Iran
5 Januari 2026
Akizungumza mwanzoni mwa kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri mjini Jerusalem, Netanyahu amesema Israel inasimama pamoja na mapambano ya wananchi wa Iran na matarajio yao ya uhuru, haki na demokrasia.
Kauli ya Waziri Mkuu huyo wa Israel ameitoa wakati maandamano makubwa yanaendelea kushuhudiwa nchini Iran, ambapo raia wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi.
Katika maelezo yake, Netanyahu pia amesema huenda dunia ikashuhudia wakati ambao wananchi wa Iran wanachukua kile alichokiita "hatma yao mikononi mwao."
Mwaka uliopita, Israel iliingia kwenye mzozo na Iran uliodumu kwa muda wa siku 12, na kwa ushirikiano na Marekani ilifanya mashambulizi yaliyolenga baadhi ya vituo muhimu vya nyuklia vya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Israel imeendelea kuushutumu uongozi wa Tehran kwa kile inachodai ni mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, jambo inaloliona kuwa tishio kwa usalama wake na wa eneo zima la Mashariki ya Kati.
Iran yatangaza posho ya kila mwezi
Wakati huo huo, mamlaka nchini Iran imetangaza jana Jumapili mpango wa kutoa posho ya kila mwezi kwa kila raia nchini humo ili kupunguza mzigo mkubwa wa kiuchumi, baada ya wiki ya maandamano.
Msemaji wa serikali Fatemeh Mohajerani ameiambia televisheni ya taifa kwamba, kila raia wa taifa hilo atapokea kiasi dola saba za Kimarekani kila mwezi, fedha ambazo zitaingizwa kwenye akaunti zao kwa kipindi cha miezi minne.
"Mpango huu utaanza kutekelezwa kuanzia Januari tarehe 10, na watu watakuwa na uwezo wa kufanya manunuzi kwa kutumia kiasi kitakachowekewa kila mwezi."
Mohajerani ameeleza kwamba kiasi hicho cha fedha kitatolewa kwa muda wa miezi minne katika mfumo wa mkopo unaoweza kutumika kununua bidhaa, lengo likiwa ni kupunguza shinikizo la kiuchumi kwa wananchi.
Mshahara wa chini nchini Iran ni takriban dola 100, huku mishahara ya wastani ya kila mwezi ikiwa karibu dola 200.
Wananchi wa Iran hutumia simu zao za mkononi pamoja na kadi za benki kufanya miamala ya kila siku badala ya pesa taslimu.
Iran inaendelea kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vikwazo vya Marekani na vya kimataifa. Mfumuko wa bei ulipanda hadi asilimia 52 mwezi Desemba, huku sarafu ya taifa ikipoteza zaidi ya theluthi moja ya thamani yake ndani ya mwaka mmoja.
Kuporomoka kwa thamani ya sarafu na kupanda kwa bei za bidhaa kumeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha, na kuchangia hali ya kutoridhika na utawala wa Tehran.
Jana Jumapili ilikuwa siku ya nane ya maandamano yaliyotokea katika takriban miji 40.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, watu wapatao 12 wamepoteza maisha wakiwemo maafisa wa vikosi vya usalama.