1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu apinga kuitambua Palestina kama taifa huru

16 Februari 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameupinga mpango wa kuitambua Palestina kama taifa huru kwa hoja kwamba uamuzi huo "utakuwa ni sawa na kuupa ushindi ugaidi."

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya mamlaka ya Palestina imesema kutambuliwa kwa Palestina kama taifa huru sio zawadi au upendeleo kutoka kwa Netanyahu bali ni haki ya msingi iliyowekwa na sheria ya kimataifa. 

Kauli ya Netanyahu ya kupinga kuitambua Palestina kama taifa huru pia imetolewa na mawaziri wenye ushawishi wa siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich, ambao wamejibu ripoti iliyochapishwa na gazeti la Marekani la The Washington Post juu ya mpango wa kuitambua Palestina kama taifa huru.

Ripoti ya The Washington Post, iliyowanukuu wanadiplomasia kadhaa wa Marekani na mataifa ya Kiarabu imeeleza kuwa mshirika mkuu wa Israel, Marekani, inashirikiana kwa karibu na mataifa ya Kiarabu juu ya mpango madhubuti wa amani na wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.

Mpango huo, kando na mambo mengine, unajumuisha pia kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.

Soma pia: Netanyahu akaidi shinikizo la kimataifa 

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameeleza kuwa, Israel inapinga kwa dhati "maagizo ya kimataifa" kuhusu suluhu ya kudumu katika mzozo wake na kundi la Hamas. Ameongeza kuwa, makubaliano ya amani yanaweza kufikiwa kwa njia ya mazungumzo ya moja kwa moja tu na bila ya masharti yoyote.

Naye Waziri wa fedha Bezalel Smotrich, anayeishi katika makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye ukingo wa magharibi, amesema taifa huru la Palestina litakuwa tishio kwa uwepo wa Israel. Suluhu ya mataifa mawili imekuwa sera kuu ya mataifa ya Magharibi katika kusuluhisha mgogoro wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.

Ama kwa upande wa mamlaka ya Palestina, wizara ya mambo ya nje ya mamlaka hiyo katika taarifa imesema kuwa taifa huru la Palestina sio zawadi au upendeleo kutoka kwa Netanyahu ila ni haki iliyowekwa na sheria ya kimataifa.

Israel yaivamia hospitali ya Nasser

Wapalestina waliojeruhiwa wakipokea matibabu katika hospitali ya Nasser mjini Khan YounisPicha: Belal Khaled/Anadolu/picture alliance

Wakati hayo yanaarifiwa, kumeibuka wasiwasi kuhusu hatima ya wagonjwa katika hospitali muhimu ya Nasser ukanda wa Gaza baada ya jeshi la Israel kuivamia leo. Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema kuwa, wagonjwa watano wamefariki hospitalini humo kutokana na ukosefu wa hewa ya oksijeni.

Wizara hiyo imeeleza kuwa, umeme ulikatika na majenereta yalishindwa kufanya kazi baada ya uvamizi wa Israel katika hospitali ya Nasser ambayo ni hospitali kubwa katika mji wa kusini wa Khan Yunis, ambayo bado inafanya kazi.

Shirika la madaktari wasio na mpaka limesema hali katika hospitali hiyo ni mbaya, na kueleza kuwa baadhi ya madaktari wamelazimika kutoroka na kuwaacha wagonjwa.

Soma pia: Jeshi la Israel lawakamata "wapiganaji wa Hamas" hospitali 

Kwengineko, Kiongozi wa kundi la Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah amesema kuwa shambulio la Israel lililosababisha vifo vya raia kadhaa kusini mwa Lebanon lilifanywa kimakusudi.

Nasrallah ameapa kuwa Israel italipa kwa damu kutokana na vifo hivyo vya raia 10 waliouawa wiki hii.

Ameongeza kuwa, kundi lake lina makombora yenye uwezo wa kuishambulia Israel na kufika umbali wa hadi kusini mwa Israel, akiutaja hasa mji wa kitalii wa Eilat ulioko kwenye pwani ya bahari ya Sham.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW