1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu apinga mashtaka dhidi yake

Oumilkheir Hamidou
22 Novemba 2019

Benjamin Netanyahu amegeuka kuwa waziri mkuu wa kwanza Israel kufunguliwa mashitaka akiwa madarakani, kwa tuhuma za kuhusika na rushwa. Kiongozi huyo anapingakwa kusema ni njama ya mapinduzi dhidi yake na hatong'atuka. 

Israel | Benjamin Netanjahu
Picha: AFP/G. Tibbon

Tangazo la kushtusha linaambatana na vurugu za kisiasa zinazoikumba Israel ambayo kwa miezi sasa haina serikali imara. Halikadhalika wananchi huenda wakatakiwa wateremke vituoni kupiga kura kwa mara ya tatu katika kipindi cha mwaka mmoja.

Baada ya miezi kadhaa ya eti eti, mwendesha mashitaka mkuu Avichai Mandelblit amemfungulia mashtaka Netanyahu - ambaye ni waziri mkuu wa muda mrefu zaidi Israel - kwa tuhuma za kupokea hongo, udanganyifu na kuvunja uaminifu.

Netanyahu hajakawia kujibu katika hotuba kali ya dakika 15, akivituhumu vyombo vya sheria, polisi  na wengineo kula njama dhidi yake na kumsingizia  uwongo ulioshawishiwa kisiasa .

"Kinachojiri hapa ni njama ya mapinuzi dhidi ya waziri mkuu "amesema Netanyahu kupitia televisheni. Lengo ni kuwa na serikali bila ya mrengo wa kulia." 

Mwendesha mashtaka mkuu Israel Avichai Mandelblit Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Schalit

Amedhamiria kuendelea kama waziri mkuu wa mpito licha ya uwezekano wa kufunguliwa kesi haraka na shinikizo la wanaomtaka ajiuzulu.

Grant amtoleo wito Netanyahu kujiuzulu

Mpinzani wake wa kisiasa Benny Gantz, aliyejaribu kuunda serikali ya muungano amesema "ni siku ya huzuni  kwa Israel kumuona kiongozi wake anashitakiwa." Hata hivyo amemtolea wito Netanyahu ajiuzulu ili apate kujiandaa kukabiliana na mashitaka dhidi yake.

"Hakuna njama yoyote ya maapinduzi, unang'ang'ania madaraka tu" amesema Banny Gantz.

Kufunguliwa mashitaka Netanyahu kunawaeza kukorofisha wadhifa wake, katika wakati ambapo wabunge wa Israel wamebakiwa na wiki tatu tu kumteua waziri mkuu atakaepata uungwaji mkono wa angalau wabunge 61 katika bunge (Knesset) lenye viti 120.

Kwa mujibu wa sheria za Israel, Benjamin Netanyahu anaweza kuendelea na wadhifa huo licha ya kushitakiwa, lakini hatoweza kuchaguliwa kuwa waziri katika serikali yoyote ile ya muungano.

Benny Gantz  amepata nguvu kutokana na kufunguliwa mashitaka Benjamin Netanyahu. Kiongozi huyo wa zamani wa vikosi vya wanajeshi amekuwa akijaribu kuwatanabahisha wabunge wa chama cha Likud, wajiunge na serikali ya umoja wa taifa - lakini hadi wakati huu hakuna aliyejitokeza.

Vyanzo: (afp,ap)