1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Netanyahu apuuza miito ya usitishwaji mapigano

31 Oktoba 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametupilia mbali miito ya usitishwaji mapigano dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Israel Tel Aviv  Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na wanahabari mjini Tel Aviv:29.10.2023Picha: Xinhua/IMAGO

Netanyahu amesema wito wa usitishwaji mapigano ni sawa na kuitaka Israel kujisalimisha kwa kundi la Hamas na kuafiki ugaidi na ukatili. Amesema hilo haliwezekani na kunukuu Biblia kwamba kuna wakati wa amani na wakati wa vita, na kwamba sasa ni wakati wa vita ili kuandaa mustakabali wa pamoja.

Kwa upande mwingine Marekani imesema haiungi mkono miito ya  usitishwaji mapigano  kwa sasa na  kusema badala yake kunaweza kuzingatiwa usitishwaji wa muda ili kuruhusu usafirishaji wa misaada.

Israel ambayo tayari imeanza mashambulizi ya ardhini na kuendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la Hamas, imerudia onyo la kuwataka raia kuondoka kaskazini mwa Gaza na kuelekea eneo la kusini. Hata hivyo baadhi ya mashuhuda wamesema vikosi vya Israel vimeshambulia barabara kuu inayoelekea eneo hilo la kusini mwa Gaza.

Eneo la Gaza likishambuliwa na vikosi vya Israel: 30.10.2023Picha: Menahem Kahana/AFP

Umoja wa Mataifa pamoja na wauguzi huko Gaza wamejawa na wasiwasi kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi karibu na hospitali. Jeshi la Israel limewataka watu waliojihifadhi kwenye hospitali ya Al Quds na katika kitongoji cha Ta al- Hawa waondoke kwenye maeneo hayo, lakini wakaazi hao wamesema hawana pa kwenda.

Soma pia: Gaza:Hakuna njia ya kutoka kwa Wapalestina wenye uraia pacha

Kwa upande wake Kundi la Hamas limechapisha video ya wanawake watatu waliochukuliwa mateka, jambo lililoibua hisia huko Israel na kuongeza shinikizo kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye ameapa kuwa atafanya kila aliwezalo ili kuwaokoa mateka wote.

Katika shambulio la Oktoba 7, Kundi la Hamas liliwaua watu 1,400 huko Israel na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200. Upande wa Palestina, wizara ya afya imesema watu 8,306 ndio tayari wameuawa.

Wito wa UNRWA kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe LazzariniPicha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amelionya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana kuwa Wapalestina waliozingirwa katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na shinikizo la kuhamishwa kwa lazima pamoja na adhabu ya jumla.

Philippe Lazzarini amesema pia kuwa kukatika kwa mawasiliano mwishoni mwa wiki kumezidisha ongezeko la kusambaratika kwa utulivu wa kiraia na kuonya kwamba ikiwa hilo litaendelea, litasababisha hali kuwa mbaya zaidi  na kuwa vigumu kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kufanya kazi huko Gaza.

Soma pia: Onyo la Israel lawatia hofu waliojihifadhi kwenye hospitali Gaza

UNRWA imeonya pia kwamba idadi ndogo ya misafara ya misaada inayoingia Gaza haitoshi kukidhi mahitaji ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika eneo hilo. Marekani imesema inatarajia kuongeza idadi ya misafara ya misaada kupitia kivuko cha Rafah kuelekea Gaza hadi kufikia malori 100 kwa siku

Lazzarini amesisitiza kuwa mfumo uliowekwa wa kuruhusu misaada kuingia Gaza unaelekea kushindwa ikiwa hakutakuwa na dhamira ya kisiasa ya kuongeza idadi ya misaada inayolingana na mahitaji ya kibinadamu.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW