Netanyahu atabiriwa kushinda uchaguzi Israel
2 Novemba 2022Waziri mkuu huyo wa zamani Benjamin Netanyahu aliwaambia wafuasi wake kwenye mkutano wa hadhara kwamba ingawa bado hawajajua matokeo ya mwisho, lakini wanaukaribia ushindi mkubwa na kuwahakikishia ataunda serikali ya mrengo wa kulia.
Matokeo yaliyotoka kwenye baadhi ya vituo vya kupgia kura yameonyesha chama cha Netanyahu cha Likud kikiongoza, hii ikiwa ni kulingana na taarifa zilizotolewa jana usiku baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika. Vyombo kadhaa vya habari vya Israel vilisema Likud na washirika wake wanaonekana kupata viti vingi vya bunge la Knesset lenye viti 120 huku vikimuweka mgombea wa chama cha Religious Zionism, Itamar Ben-Gvir nafasi ya tatu.
Soma Zaidi: Israel kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya
Mapema jana baada ya kupiga kura mjini Jerusalem, Netanyahu aliyeongozana na mkewe Sarah alisema ingawa alikuwa na wasiwasi, lakini kwa msaada wa kila mmoja aliyewasilikia ana matumaini ya kupata matokeo mazuri. Na kuhusiana na wasiwasi wa jamii ya kimataifa kwamba ataunda serikali ya mrengo wa kulia, Netanyahu alisema chama na muungano wake wataunda serikali isiyokuwa na msingi wa Udugu wa Kiislamu, ambao amesema unaunga mkono ugaidi.
"Hatutaki serikali ya pamoja na Udugu wa Kiislamu ambayo inaunga mkono magaidi na kukana uwepo wa Israel, ambao pia wanaichukia sana Marekani," Alisema Netanyahu.
Muungano wa serikali ya mpito ya waziri mkuu Yair Lapid wa ulitarajiwa kushika nafasi ya pili, ingawa kuna uwezekano wa mabadiliko wakati matokeo ya mwisho yatakapotolewa baadaye wiki hii.
Netanyahu ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya ufisadi, amekuwa akiangazia fursa ya kurejea kwenye uwanja wa siasa. Aliondolewa na muungano wa Lapid baada ya miaka 12 ya kuwa mamlakani. Muungano huo uliodumu kwa muda, ulivileta pamoja vyama vinane vya siasa, kutoka mirengo ya kulia na kushoto pamoja na chama huru cha Kiarabu.
Soma Zaidi: Je Netanyahu kufutiwa kesi ya rushwa inayomkabili?
Wachambuzi wanatarajia kinyang'anyiro kikali katika uchaguzi huo, ambao mara nyingi hutegemea uungwaji mkono wa vyama vidogovidogo ili kupata wingi wa kutosha bungeni. Tofauti na matarajio, raia wengi walijitokeza kupiga kura, idadi ya juu kabisa kushuhudiwa tangu uchaguzi wa mwaka 1999.
Mchambuzi wa sayansi ya siasa Gideon Rahat katika Taasisi ya Demokrasia ya Israel ameiambia DW kwamba kinyang'anyiro hicho kinaashiria mgawanyiko wa kisiasa nchini humo. Amesema inaashiria siasa zimegawanyika mno, na uchaguzi huu sasa unaonekana tu ni wa vyama vya siasa na si wapiga kura na kwamba kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara kunaonyesha dhahiri kwamba wako katika hali ambayo huenda haiwezi kupatiwa suluhu kwa kufanya uchaguzi.
Mashirika: DW/AFPE