1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aungwa mkono kuunda serikali

Deo Kaji Makomba
7 Mei 2020

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameungwa mkono rasmi na idadi kubwa ya wabunge kuongoza serikali mpya Alhamisi (07.05.2020). Bunge la Israel limeridhia serikali mpya ya mseto.

Russland Moskau Benjamin Netanjahu
Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Chama cha Likud na chama cha Buluu na Nyeupe vilitoa taarifa vikisema kuwa vimempa rais wa nchi hiyo saini za wabunge 72 wakimpendekeza Nyetanyahu kuwa Waziri mkuu. Pindi atakapoidhinishwa na Rais Reuven Rivlin, Nyetanyahu atakuwa na kipindi cha wiki mbili kuunda serikali yake.

Bunge la Israel, Knesset, lilipitisha sheria mapema siku ya Alhamisi kupitisha mfumo mpya wa serikali ya muungano kati ya Nyetanyahu na Gantz kushiriki pamoja katika nafasi ya uongozi ya uwaziri mkuu na kuhitimisha mwaka mzima wa mkwamo wa kisiasa.

Sheria ambayo ilipitishwa kiurahisi kwa kura 72 dhidi ya 36, imekuja siku moja baada ya mahakama ya juu ya Israel kutoa uamuzi kwamba haitaingilia mpangilio mpya au kumzuia Netanyahu kuongoza serikali licha ya mashitaka ya ufisadi yanayomkabili.

Uamuzi huo kimsingi ulimaliza mgogoro wa kisiasa na kuiepusha Israel kuingia katika uchaguzi wa nne katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja hivi.

Baada ya kupambana katika chaguzi tatu ambazo hazikutoa mshindi wa moja kwa moja mwaka uliopita, na uchunguzi wa maoni ukibashiri mkwamo wa kisiasa kuendelea kuwepo, Netanyahu na Gantz, mkuu wa zamani wa jeshi, walitangaza mwezi uliopita kuwa wataunganisha nguvu kuiongoza nchi hiyo katika kukabiliana na mripuko wa janga la virusi vya Corona pamoja na kuzitafutia ufumbuzi athari kubwa za janga hilo kwa uchumi.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kulia, na Benny GantzPicha: Reuters/A. Cohen

Wakosoaji na vikundi vinavyopigania utawala bora walisema kuwa mpango wao haukuwa halali kisheria na wakawasilisha kesi katika mahakama ya juu kabisa ya Israel.  Walihoji kwamba sheria inapaswa kumzuia afisa aliyeshitakiwa na uhalifu mkubwa asiendelea kuwa waziri mkuu. Walipinga pia kuanzishwa kwa nafasi mpya ya waziri mkuu ya kupokezana, ambayo ingemruhusu Netanyahu kubaki madarakani wakati wote wa kesi yake ya ufisadi na hata kipindi cha kusikilizwa rufaa.

Nafasi hiyo mpya itafaidi haki zote za waziri mkuu ikiwemo makazi rasmi na msamaha wa kisheria ambayo inawataka wafanyakazi wa umma ambao sio Waziri mkuu kujiuzulu endapo watashitakiwa kwa kosa la jinai, jambo ambalo ni muhimu sana kwa Netanyahu.

Zaidi ya siku mbili za majadiliano wiki hii mahakama ilizingatia hoja kabla ya kutoa hukumu kwamba hakukuwa na sababu za msingi kisheria za kuizuia serikali kushika hatamu za kiofisi.

Netanyahu ameshitakiwa kwa udanganyifu, kukosa uaminifu na kukubali hongo katika muendelezo wa kashfa zinazojumuisha upendeleo wa kibiashara na wamiliki matajiri wa vyombo vya habari. Kesi yake inatarajiwa kuanza kusikilzwa baadaye mwezi huu.

Netanyahu amekuwa akikanusha shutuma hizo, na tangu kesi yake ilipoanza msimu uliopita wa mapukutiko, amekuwa mara kwa mara akiukosoa mfumo wa sheria wa Israel.

(ap)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW