Netanyahu kuhutubia Bunge Marekani
24 Julai 2024Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina waliingia katika sehemu ya jengo la Bunge wakati Benjamin Netanyahu akijiandaa kuyahutubia mabaraza yote mawili ya Bunge la Congress leo Jumatano. Waziri Mkuu huyo wa Israel yuko Marekani kufuatia mwaliko aliopewa na viongozi wa mabaraza hayo.
Polisi wanaolinda bunge hilo wamesema baada ya waandamanaji kukaidi wito wa kuondoka katika eneo hilo, wamelazimika kuwatawanya kwa nguvu.
Soma zaidi: Netanyahu yuko Washington kukutana na viongozi wa Marekani
Netanyahu atahutubia bunge la Marekani wakati akikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa Rais wa Marekani Joe Biden na baadhi ya wanachama wa ngazi za juu wa chama cha Biden juu ya namna anavyoendesha vita katika Ukanda wa Gaza.
Netanyahu atatoa hotuba yake akiwa ameambatana na ndugu wa mateka wanaoshikiliwa na kundi la Hamas waliokamatwa katika mashambulizi ya Oktoba 7.
Kulingana ripoti za vyombo vya habari, kiongozi huyo wa Israel anatarajiwa kukutana na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris.
Naye mgombea wa urais wa nchi hiyo kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump anatazamiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu huko Palm Beach Florida.
Ziara ya Netanyahu inajiri wakati Israel ikiyalaani makubaliano yaliyosimamiwa na China Jumanne yanayolenga kuliingiza kundi la Hamas katika serikali ya Umoja wa kitaifa mara vita vitakapokwisha kwenye ukanda huo.
Huduma ya Intaneti yarejeshwa hospitali Ukanda wa Gaza
Hayo yakiendelea, Murugenzi mkuu wa kampuni ya Space X Elon Musk kupitia jukwaa la X amesema huduma ya mtandao wa intaneti iimerejeshwa tena katika hospitali moja katika Ukanda wa Gaza kupitia kampuni yake yake ya mawasiliano na Starlink ikishirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Akimshukuru Musk, waziri wa mambo ya kigeni wa falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan amesema, huduma hiyo ya intaneti yenye kasi kubwa itawezesha maisha ya watu kuokolewa kwa wataalamu wa afya kutoa huduma kwa njia ya video.
Wakati huo huo, wizara ya afya chini ya kundi la Hamas imesema kuwa idadi ya watu waliouwawa tangu ulipoanza mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas ni zaidi ya watu 39,100
Idadi hiyo inajumuisha vifo vya watu 55 vilivyotokea ndani ya saa 24. Mamlaka hiyo imeongeza pia kuwa, watu wasiopungua 90,000 wamejeruhiwa Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7.