1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kushiriki tena mazungumzo ya kusitisha vita Gaza

4 Julai 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin anakutana na baraza lake la usalama Alhamis jioni kujadili misimamo mipya ya Hamas kuhusu usitishaji vita Gaza, huku Hezbollah likivurumisha mamia ya maroketi na droni dhidi ya taifa hilo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameripotiwa kukubali kutuma wajumbe wa majadiliano kufufua mazungumzo ya kusitisha vita Gaza.Picha: Cohen-Magen/REUTERS

Israel ilipokea majibu ya Hamas jana Jumatano kuhusu pendekezo lililotolewa mwishoni mwa mwezi Mei na Rais wa Marekani Joe Biden, ambalo linahusisha kuwachiwa kwa mateka wapatao 120 wanaoshikiliwa Gaza na usitishaji vita katika eneo hilo la Palestina.

Afisa wa Palestina alie karibu na juhudi za upatanishi amesema Hamas imeonyesha utayari wa kulegeza msimamo kuhusu baadhi ya vipengele, ambavyo vitaruhusu kufikiwa kwa msingi wa makubaliano ikiwa Israel itaridhia.

Katika Ukanda wa Gaza, Wapalestina wamepoeka hatua hiyo kwa tahadhari kuelekea jibu la Israel. Mkaazi mmoja aliejitambulisha kwa jina la Youssef, ambaye ni baba wa watoto wawili aliehamia Khan Younis, alieleza matumaini kuwa huu utakuwa mwanzo wa kumalizika kwa vita, akisema wamechoshwa na vita hivi.

Wakaazi wa Gaza wamepokea juhudi mpya kwa tahadhari wakitumai zitakuwa mwanzo wa mwisho wa vita.Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Soma pia: Kiongozi wa Hamas azungumza na wapatanishi kuhusu usitishaji vita Gaza

Wizara ya afya ya Gaza imesema leo kuwa idadi ya vifo vya Wapalestina katika vita hivyo vya karibu miezi tisa imevuka 38,000, huku wengine 87,445 wakiwa wamejeruhiwa.

Akizungumza kwenye mkutano usiyo wa kawaida wa wanachama wa kudumu wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu mjini Cairo, mwakilishi wa Palestina kwenye jumuiya hiyo, Mohannad al-Aklouk, ameyataka mataifa ya Kiarabu kuchukua hatua dhidi ya Israel.

"Hii leo, zaidi ya wakati wowote hapo kabla, nadhani mataifa ya Kiarabu yaangalie uhusiano wao na Israeli na uhalifu wake dhidi ya watu wa Palestina kwa mtazamo tofauti," alisema Mohannad al-Aklouk.

"Lugha ya kulaani na kuipigania (Palestina) kwa maneno matupu havitoshi ikiwa havitafuatiwa na hatua za kiuchumi, kisheria, kisiasa na kidiplomasia zinazoifanya Israel na dunia kuchukulia suala hilo kwa uzito."

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

02:03

This browser does not support the video element.

Hezbollah yavurumisha maroketi Israel

Wito wake umekuja huku mvutano ukipamba moto katika mpaka wa kaskazini wa Israel na Lebanon, ambapo kundi la wanamgambo wa Hezbollah limesema kuwa limevurumisha zaidi ya roketi 200 na droni za milipuko dhidi ya maeneo 10 ya jeshi la Israel, katika mfululizo wa kulipiza kisasi cha mauaji ya kamanda wake Mohammad Nasser, jana Jumatano kusini mwa Lebanon.

Soma pia: Itachukuwa miaka 16, dola bilioni 40 kuijenga tena Gaza - UM

Jeshi la Israel limesema karibu vitupo 200 na vifaa vingine 20 vya angani vilionekana vikivuka kutoka Lebanon na kuingia ardhi ya Israel, na kuongeza kuwa idadi kadhaa vilizuwiwa na mifumo ya ulinzi wa anga na ndege za jeshi.

Afisa wa juu wa Hezbollah Hashem Safieddine, akizungumza mjini Beirut kwenye tukio la kumkumbuka Nasser, aliashiria kuwa kundi lake litapanua shabaha zake.

Marekani imekuwa ikiongoza juhudi za kidiplomasia kutuliza mzozo huo, lakini Hezbollah imesema haitositisha mapigano wakati Israel ikiendelea na mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW