1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: Majeshi ya Israel kusalia Mlima Hermon

18 Desemba 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema wanajeshi wake wataendelea kubaki katika eneo la kimkakati la Mlima Hermon kwenye mpaka wa Syria hadi mpango mwingine utakapofikiwa kutahakikisha usalama wa Israel.

Nahostkonflikt - Israel billigt Waffenruhe mit Hisbollah
Picha: Uncredited/Israeli Government Press Office/AP/dpa/picture alliance

Jana Jumanne, Netanyahu alilitembelea eneo hilo na kufanya mazungumzo na maafisa wa usalama pamoja na makamanda wa jeshi.

"Niko hapa kwenye kilele cha Mlima Hermon pamoja na Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi, Kanali wa Kamandi ya Kaskazini, mkuu wa Shin Bet, na makamanda wakuu. Tuko hapa katika wakati muhimu kuamua juu ya utayari wa Israel mahali hapa muhimu hadi pale mpango mwingine utakapofikiwa unaohakikisha usalama wa Israel," alisema Netanyahu.

Israel ilichukua udhibiti wa eneo la kusini mwa Syria kwenye mpaka na eneo la mlima Golan siku chache baada ya Rais Bashar Al-Assad kuondolewa madarakani na waasi.

Maafisa wameeleza hatua hiyo kuwa ya muda tu ili kuhakikisha usalama wa mipaka ya Israel lakini hawajatoa dalili yoyote ya muda ambao wanajeshi hao watasalia.

Wiki iliyopita, waziri wa ulinzi Israel Katz aliagiza wanajeshi kujiandaa kubaki kwenye eneo la mlima Hermon katika msimu wa baridi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW