1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: Tutashambulia kila eneo la Iran

14 Juni 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake itashambulia kila "eneo na shabaha" ya utawala wa Iran.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (katikati) na viongozi kadhaa wa usalama
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (katikati) na viongozi kadhaa wa usalama.Picha: Avi Ohayon (GPO)/Handout/Anadolu/picture alliance

Ametoa matamshi hayo saa chache baada ya waziri wake wa ulinzi Israel Katz kuionya Iran kuwa mji wake mkuu "utawaka moto" iwapo itaendelea kuvurumisha makombora ya masafa kuelekea Israel. 

"Tutashambulia kila eneo, kila shabaha ya utawala wa Ayatollah (Ali Khamenei)," amesema Netanyahu katika ujumbe wa video ulitolewa siku ya Jumamosi.

Netanyahu na kuongeza kuwa Israel "imefanya uharibifu mkubwa kwenye mradi wa nyuklia wa Iran" baada ya mashambulizi yake ya siku ya Ijumaa.

Wakati hayo yakiripotiwa Iran imethibitisha Jumamosi jioni kuwa Israel imemuua Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Iran Meja Habibollah Akbarian na kamanda mwingine wa ngazi ya juu. 

Taarifa hizo zimetolewa wakati hali ya wasiwasi ikizidi kutanda baada ya pande hizo mbili hasimu kushambuliana vikali siku ya Jumamosi. 

Shirika la Habari la ISNA limeripoti mkuu huyo wa polisi ya Iran aliuwawa kwa shambulizi la droni Jumamosi asubuhi huko katika mji mdogo wa Asadabad umbali wa kilometa 300 kutoka mji mkuu, Tehran, wakati Israel ilipoendeleza hujuma zake dhidi ya Iran kwa siku ya pili mfululizo. 

Hilo ni pigo jingine kubwa kwa Iran ambayo tangu jana tayari imepoteza viongozi wake kadhaa wa vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Mkuu wa Majeshi na Kiongozi wa Kikosi Maalumu cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran waliouawa katika mashambulizi ya Israel. 

Katz: Tehran itawaka moto makombora ya Iran yakiendelea 

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz.Picha: Alessandro Di Meo/ANSA/ZUMA Press/picture alliance

Mapema leo Jumamosi Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz ameyatoa matamshi hayo baada ya kufanya tathmini ya uharibifu uliofanywa na mashambulizi ya makombora ya masafa yaliyofyetuliwa na Iran usiku wa Ijumaa na Jumamosi alfajiri kujibu hujuma nzito za Israel dhidi ya miundombinu yake ya nyuklia na vituo vya kijeshi. 

Mashambulizi hayo yamewaua watu wasiopungua watatu nchini Israel na kuharibu majengo ya maakazi kwenye miji kadhaa husasani mji mkuu Tel Aviv. Katz amesema Iran italipa gharama kubwa kwa kuwadhuru raia wa Israel.  

Amemnyooshea kidole cha lawama Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ambaye aliapa jana Ijumaa kuwa Iran itajibu vikali mashambulizi ya Israel kwenye ardhi yake. 

"Dikteta wa Iran anawaingiza hatarini raia wa Iran na kufungua mlango wa jambo ambalo -- hususani wakaazi wa Tehran -- watalipia gharama kubwa kwa sababu ya uhalifu unaotendwa dhidi ya raia wa Israel," amesema Katz katika taarifa iliyonukuliwa na mashirika ya habari ya kimataifa.

"Iwapo (Ayatollah Ali) Khamenei ataendelea kufyetua makombora kuyalenga maeneo muhimu ya Israel -- Tehran itawaka moto." 

Afisa wa Iran asema nchi hiyo ilihamisha vifaa vyake vya nyuklia kituo cha Fordo 

Katika hatua nyingine Israel imeendelea kufanya mashambulizi ndani ya Iran huku ripoti za hivi karibuni zikisema ndege zake za kivita zimekilenga kituo cha kusafisha mafuta cha Iran cha Tabriz.

Mikanda ya video imeonesha wingu zito la moshi limetanda kwenye kituo hicho. Mashambulizi hayo ni mwendelezo wa hujuma za Israel ndani ya Iran zilizoanza siku ya Ijumaa. 

Kituo cha nyuklia cha Iran cha Fordo.Picha: picture alliance/dpa/Satellite image 2019 Maxar Technologies/AP

Wakati huo huo afisa mmoja wa Iran amesema nchi hiyo ilihamisha vifaa vyake muhimu na vya kimkakati kutoka kwenye kituo chake cha nyuklia cha Fordo kabla ya Israel kukishambulia. 

Afisa huyo Behrus Kamalwandi ambaye ni msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amesema uharibifu uliotokea nje ya kituo hicho hauna athari kubwa na unaweza kushughulikiwa.

Akinukuliwa na Shirika la Habari la Iran, IRNA, Kamalwanfi amesema sehemu kubwa ya vifaa na malighafi muhimu vilihamishwa kwenda eneo salama. 

Kituo cha nyuklia cha Fordo kinajumisha mitambo ya kurutubisha madini ya urani na kikakutikana kiasi kilometa 100 kutoka mji mkuu wa Iran, Tehran.

Kituo hicho kimejengwa chini kabisa ya mlima mkubwa na kinalindwa na mizinga ya kijeshi. 

Iran yajibu mapigo dhidi ya Israel usiku wa Ijumaa

Mashambulizi ya angani yaliyotekelezwa na Israel dhidi ya Iranna mashambulizi ya kulipa kisasi kutoka Tehran yamesababisha vifo vya mamia, uharibifu mkubwa, na kutishia kulipuka kwa vita kamili Mashariki ya Kati.

Israel ilitumia ndege za kivita pamoja na droni zilizosafirishwa kwa siri hadi ndani ya Iran kushambulia maeneo nyeti na kuua majenerali na wanasayansi wa juu wa kijeshi.

Israel ilisema mashambulizi hayo yalikuwa ya lazima kabla Iran haijafikia hatua ya kutengeneza silaha ya nyuklia, ingawa Marekani na wataalamu wa kimataifa walikuwa wamekadiria kuwa Tehran haikuwa ikifanyia kazi silaha hiyo kwa wakati huo.

Haya yalijiri siku chache kabla ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran kuhusu mpango wa nyuklia, na sasa yameingia katika hali ya sintofahamu.

Mandhari ya uharibifu baada ya kombora la Iran kupiga karibu kabisa na Wizara ya Ulinzi mjini Tel Aviv, Israel, mnamo Juni 13, 2025.Picha: Saeed Qaq/Anadolu/picture alliance

Iran ilijibu kwa kurusha droni na makombora ya balistiki kuelekea Israel, ambapo milipuko ilirindima angani usiku katika miji ya Tel Aviv na Jerusalem, huku watu wakikimbilia mafichoni.

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema katika ujumbe wa video: "Hatutaruhusu wakimbie salama kutokana na jinai hii kubwa." Iran ilisema watu 78 waliuawa na zaidi ya 320 kujeruhiwa kwenye mashambulizi ya Israel.

Mashambulizi ya Iran yawasha moto ndani ya Israel

Hospitali moja mjini Tel Aviv iliwatibu watu saba walioumia kwenye shambulio la pili kutoka Iran, ambapo mwanamke mmoja alifariki. Saa chache baadaye, kombora la Iran lilipiga karibu na makazi ya watu katika mji wa Rishon Lezion, na kuua watu wawili na kujeruhi 19.

Katika mji wa Tehran, milio ya milipuko na makombora ya ulinzi wa anga vilisikika usiku wa manane. Uwanja wa ndege wa Mehrabad ulishika moto, huku picha zikionyesha moshi na moto mkubwa ukitanda angani.

Idara za uokoaji za Israel ziliripoti kuwa watu 34 walijeruhiwa katika eneo la Tel Aviv, na baadhi wakiokolewa kutoka chini ya kifusi. Katika eneo la Ramat Gan, magari yaliteketea na nyumba kadhaa kuharibiwa vibaya.

Maafisa wa Marekani walisema mifumo ya ulinzi wa anga ya ardhini kutoka Marekani ilikuwa ikisaidia kuharibu makombora ya Iran kabla hayajafika.

Hofu ya vita kuu yazidi

Mashambulizi ya pande zote mbili yaliongeza wasiwasi wa kuzuka kwa vita kubwa baina ya Iran na Israel, jambo ambalo limeitumbukiza kanda hiyo kwenye machafuko zaidi. Mataifa jirani yalilaani mashambulizi ya Israel huku viongozi wa kimataifa wakitaka pande zote kujizuia.

Israel yaishambulia Iran na kulenga maeneo tofauti

01:16

This browser does not support the video element.

Hapo awali, serikali za Marekani ziliwahi kuzuia mashambulizi kama haya kwa hofu ya kuibua vita vya kikanda ambavyo haviwezi kudhibitika, hasa kwa kuzingatia ugumu wa kuharibu kabisa miundombinu ya nyuklia ya Iran ambayo imejengwa chini ya ardhi na kusambazwa maeneo mbalimbali.

Lakini mfululizo wa matukio, yakiwemo mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7, 2023, pamoja na kuchaguliwa tena kwa Rais Donald Trump, vilichangia mazingira ambayo yaliiruhusu Israel kutekeleza mpango wake. Netanyahu alisema Marekani ilijulishwa kabla ya mashambulizi.

Maeneo nyeti yashambuliwa, viongozi wa juu Iran wauawa

Israel ilisema mashambulizi yake yalihusisha ndege 200 na kushambulia maeneo 100 ya kijeshi. Shirika la ujasusi la Israel, Mossad lilitumia droni na silaha za kisasa zilizowekwa ndani ya Iran kwa siri kushambulia mfumo wa ulinzi wa anga karibu na Tehran.

Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni kituo cha kurutubisha madini ya urani cha Natanz ambako moshi mweusi ulionekana ukitanda angani. Pia, kituo kidogo cha Fordo kilishambuliwa, pamoja na kituo cha utafiti wa nyuklia cha Isfahan.

Kiwanda cha urutubishaji wa urani cha Natanz kinaelezwa kuharibiwa vibaya kwa juu na mashambulizi ya Israel.Picha: Alfred Yaghobzadeh/SalamPix/abaca/picture alliance

Msemaji wa jeshi la Israel alisema Natanz "imeharibiwa kwa kiwango kikubwa" na kwamba operesheni bado inaendelea. Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Silaha za Nyuklia (IAEA) ilithibitisha kuwa sehemu ya juu ya kituo cha Natanz imeharibiwa kabisa.

Israel yajipanga kwa mashambulizi ya muda mrefu

Uharibifu wa miundombinu ya umeme katika mtambo wa Natanz unaweza kuathiri mitambo ya ndani, hata kama haikupigwa moja kwa moja. Maafisa wa kijeshi wa Israel walisema mashambulizi hayo ya awali yalitoa nafasi ya ndege zao kuingia kwa urahisi zaidi katika anga ya Iran kwa mashambulizi ya baadaye.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Israel ilikua ikishambulia mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, ikiwemo mitambo ya kutengeneza makombora na vituo vya kurusha makombora. Israel inajiandaa kwa operesheni itakayodumu hadi wiki mbili, ingawa muda kamili haujaamuliwa.

Waliouawa ni pamoja na majenerali watatu wa juu wa Iran, wakiwemo mkuu wa majeshi Gen. Mohammad Bagheri, kiongozi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi Gen. Hossein Salami, na mkuu wa mpango wa makombora ya balistiki Gen. Amir Ali Hajizadeh.

Mamia ya watu waliobeba bendera za Palestina na Iran wakiwa katika Uwanja wa Sebin kuandamana kupinga mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na Iran, mjini Sanaa, Yemen, mnamo Juni 13, 2025.Picha: Mohammed Hamoud/Anadolu/IMAGO

Netanyahu adokeza chanzo cha mashambulizi

Netanyahu alisema mashambulizi hayo yalipangwa tangu Novemba baada ya kuuawa kwa Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah, mshirika mkubwa wa Iran. Hata hivyo, mashambulizi hayo yalicheleweshwa hadi Aprili.

Iran ilijibu kwa kutuma zaidi ya droni 100, ingawa Israel ilisema nyingi ziliharibiwa kabla ya kuingia kwenye anga yake. Israel pia ilitangaza kuwaita askari wa akiba na kupeleka wanajeshi maeneo mbalimbali nchini wakitarajia mashambulizi zaidi kutoka Iran au washirika wake kama Hezbollah.

Rais Donald Trump aliiambia Iran kupitia mtandao wake wa Truth Social kwamba lazima wafikie makubaliano ya nyuklia na Marekani kabla hali haijawa mbaya zaidi. "Iran lazima ifanye makubaliano, kabla ya kubakia bila chochote na kupoteza fahari ya Ufalme wao wa zamani," aliandika.

Wakati huo huo, Jordan ilifungua tena anga yake asubuhi siku ya Jumamosi, baada ya kuifunga kwa siku moja kutokana na hali ya wasiwasi kati ya Israel na Iran.

DW inaendelea kufuatilia hali inavyojitokeza Mashariki ya Kati na kukuletea taarifa kadiri zinavyotufikia.

Chanzo: APE, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW