1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu: Upatanishi wa Qatar unaleta matatizo

25 Januari 2024

Qatar imesema kuwa imeshangazwa na matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yaliyovujishwa Jumatano, ambapo alizikosoa juhudi za upatanishi za nchi hiyo na Hamas.

Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo vikosi vya Israel vinafanya operesheni ya ardhini katika mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis.

Katika mkutano na famili za mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas, Netanyahu amesema dhima ya Qatar katika juhudi za upatanishi inaleta "matatizo." Katika matamshi hayo ya Netanyahu yaliyovujishwa na ambayo yaliyorushwa katika televisheni moja ya Israel, waziri mkuu huyo aliziambia familia hizo za mateka kwamba, kwa makusudi hajaishukuru Qatar kwa juhudi zake, akisema huenda hilo likaweka shinikizo zaidi kwa kundi la Hamas ambalo Marekani, Umoja wa Ulaya Ujerumani ikiwemo na mataifa mengine yamelitaja kuwa kundi la kigaidi.

Mwenyeji wa viongozi wa Hamas walio uhamishoni

Netanyahu aliendelea kusema kwamba, mtazamo wa Israel kwa Qatarni sawa na mtazamo wake kwa Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu kwa kuwa mashirika hayo yana upendeleo na hayasaidii vya kutosha katika kuhakikisha kwamba mateka wanaachiliwa huru.

Moshi ukifuka baada ya shambulizi Khan YounisPicha: Mohammed Dahman/AP Photo/picture alliance

Katika sauti hiyo iliyovujishwa, Netanyahu amesikika akisema pia alielezea ghadhabu zake kwa Marekani kwa hatua yake ya kuweka kambi ya kijeshi nchini Qatar. Anasema amewaambiwa Wamarekani waliwekee shinikizo taifa hilo la Ghuba ili nalo lilishinikize kundi la Hamas.

Qatar, mapatanishi mkuu na nchi yenye mahusiano ya karibu na kundi la Hamas ni mwenyeji wa baadhi ya viongozi wa kundi hilo waliokimbilia uhamishoni na imesema matamshi ya Netanyahu yanaonyesha ni ya "kutowajibika na ya uharibifu."

Haya yanafanyika wakati ambapo mazungumzo muhimu yanaendelea katika juhudi zua kuendeleza makubaliano ambayo huenda yakapatikana, na ambayo huenda yakaleta utulivu katika vita hivyo vilivyodumu kwa miezi mitatu sasa.

Israel sharti ikubalie misaada kuingia Gaza

Wakati huo huo, makombora ya angani ya Israel na opereshenizake za ardhini leo zinaelekezwa katika mji wa Gaza wa Khan Younis, ambapo Umoja wa Mataifa unasema watu tisa waliuwawa kutokana na mashambulizi ya vifaru yaliyofanywa na majeshi ya Israel hapo jana.

Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza David CameronPicha: dpa/PA Wire/picture alliance

Afisi ya habari ya kundi la Hamas pia imeripoti makabiliano makali katikati na magharibi mwa Khan Younis, huku wizara yake ya afya ikiripoti vifo kadhaa kutokana na mashambulizi ya usiku kucha katika mji huo na kwengineko katika eneo hilo. Wizara hiyo ya afya imesema pia watoto 4 wameuwawa katika kambi ya Nuseirat kwenye shambulizi la mapema leo.

Kwengineko waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron amesema amemwambia Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa ni sharti malori zaidi ya yakubaliwe kuingia Gaza na kuwepo na usitishwaji wa mapigano kwa ajili ya kutolewa kwa misaada ya kiutu ili kuwasaidia walio katika hali ya kukata tamaa.

Cameron ambaye yuko ziarani Mashariki ya Kati, amefanya mikutano tofauti na Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas na ametangaza kwamba Uingereza na Qatar zinashirikiana kuhakikisha kwamba misaada zaidi inaingia Gaza.

Vyanzo: Reuters/AFPE/APE https://www.dw.com/en/israel-hamas-war-khan-younis-encircled-as-israel-mourns/live-68068833