1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: Walowezi wenye vurugu ni wachache

17 Novemba 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vurugu za walowezi dhidi ya Wapalestina na Jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi, huku akisema kuwa wahusika ni wachache.

Israel Jerusalem 2022 | Benjamin Netanjahu bei Protesten gegen die Regierung Bennett
Picha: Menahem Kahana/AFP

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali Netanyahu amenukuliwa akiliambia baraza la mawaziri kwamba  "Wengi wa walowezi ni "watii wa sheria na waaminifu kwa taifa.” Netanyahu alisema serikali yake itachukua "hatua kali sana dhidi ya” wale wanaohusika na "vurugu, dhidi ya IDF na dhidi ya Wapalestina kwa sababu wao ni taifa la kisheria, na taifa la sheria hutenda kwa mujibu wa sheria.

Ikimbukwe Ijumaa iliyopita shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilikemea kile ilichosema ni mashambulizi yanayoongezeka ya walowezi wa Kiyahudi wenye msimamo mkali dhidi ya mali na nyumba za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu ongezeko la vurugu

Msemaji mjini Geneva wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) alisema kuna tabia ya ongezeko la vurugu dhidi ya Wapalestina. Watu kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo, ikiwemo kiwanda cha maziwa. Mashambulizi zaidi ya 260 yalirekodiwa mwezi Oktoba, zaidi ya idadi ya mashambulizi katika mwezi mmoja tangu 2006.

Wapalestina waliokimbia makazi yao waliweka mahema yao miongoni mwa vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na jeshi la Israeli, katika kambi ya wakimbizi ya Bureij, katikati mwa Ukanda wa Gaza Novemba 10, 2025.Picha: Eyad Baba/AFP/Getty Images

Israel mara kwa mara hukataa tuhuma za Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN na kuishutumu kuwa na upendeleo. Katika Vita vya Siku Sita vya mwaka 1967, Israel ilichukua udhibiti wa Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

Wayahudi laki saba na Wapalestina milioni tatu wanaishi eneo tete

Rekodi za sasa zinaonesha, takriban walowezi wa Kiyahudi 700,000 wanaishi huko wakiwa miongoni mwa Wapalestina milioni 3. Wapalestina wanadai maeneo hayo kwa ajili ya taifa la baadaye lenye Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake.

Tangu mashambulizi ya kigaidi kutoka Ukanda wa Gaza dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, zaidi ya Wapalestina 1,000 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki, katika operesheni za vikosi vya usalama vya Israel na mashambulizi ya walowezi.

Jumla ya Waisrael 59 waliuawa huko katika uvamizi au mapigano katika kipindi hicho hicho.

Netanyahu na apizo lake la kupinga taifa la Palestina

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Netanyahu ameapa kupinga jaribio lolote la kuanzisha taifa la Palestina, siku moja kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura kuhusu azimio lililoandaliwa na Marekani kuhusu Gaza, ambalo linaacha mlango wazi katika uwezekano wa uhuru wa Palestina.

Netanyahu pia alikataa marejeleo yoyote katika pendekezo la Marekani kuhusu kuondoa silaha Gaza. Katika taarifa yake hiyo ya Jumapili nayo pia kwa baraza lake la mawaziri alibainisha kuwa pendekezo hilo linataka Gaza iwe bila silaha na Hamas ipokonywe silaha.

Kimsingi Baraza la Usalama linatarajiwa kupiga kura kuhusu pendekezo la Marekani la kutoa mamlaka ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuanzisha kikosi cha kimataifa cha kudumisha utulivu Gaza, licha ya upinzani kutoka Urusi, China na baadhi ya nchi za Kiarabu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW