1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu, Zelensky ziarani nchini Marekani

Grace Kabogo DPA, AFP, AP, Reuters
28 Julai 2026

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky wamewasili Washington, Marekani ambapo Jumanne wanatarajiwa kuhudhuria ibada ya kumuaga Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham.

Picha ya pamoja | Trump, Zelensky, Netanyahu
Zelensky na Netanyahu kukutana na Trump kwa nyakati tofauti mjini WashingtonPicha: picture alliance

Graham alikuwa mtetezi mkubwa wa maslahi ya Israel na Ukraine. Ziara hiyo pia inaweza kuwapa fursa viongozi hao kukutana na Rais Donald Trump. Huo utakuwa mkutano wa kwanza kati ya Trump na Netanyahu tangu Marekani na Israel zianzishe mashambulizi dhidi ya Iran, wakati tofauti kati yao kuhusu kuendeleza vita au kutafuta suluhisho la kidiplomasia zikizidi kujitokeza.

Trump alimkaribisha Netanyahu kwa mara ya mwisho katika Ikulu ya White House mwezi Februari. Wakati huo, mazungumzo yao yalijikita kuangazia jinsi ya kulishughulikia suala la Iran. Takriban wiki mbili na nusu baadaye, Marekani na Israel zikaanzisha mashambulizi yao ya pamoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tofauti za kimaslahi

Miezi mitano imepita na tofauti za kimaslahi kati ya Marekani na Israel kuhusu vita hivyo zimeanza kuonekana wazi zaidi. Wakati Israel ikidai kutaka kuendelea na vita, Trump ameonekana akitafuta suluhisho la kidiplomasia. Hata hivyo, kufuatia kuongezeka kwa mzozo huo hivi karibuni, makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na makubaliano ya mfumo wa maelewano kati ya Washington na Tehran sasa hayapo tena.

Akizungumza kabla ya kuelekea Washington, Netanyahu amesema anaenda kukutana na Trump, rafiki wa Israel, na huo utakuwa mkutano wao wa nane tangu Trump alipochaguliwa kuwa rais kwa muhula wake wa pili, akisema hiyo ni fursa ya kipekee na heshima kubwa sana.

Mlango Bahari wa Hormuz umekuwa moja ya njia hatari za majini tangu Machi, wakati Iran ilipoanza kuzishambulia meliPicha: REUTERS

''Tutajadiliana masuala yote muhimu yaliyoko katika ajenda, hasa suala la Iran. Bila shaka lengo letu ni kuhakikisha tunalinda usalama wetu huku pia tukipanua wigo wa amani katika eneo letu,'' alifafanua Netanyahu.

Kulingana na Netanyahu, pia jambo jingine linalompeleka Washington ni kutoa heshima zake za mwisho kwa rafiki yake wa kweli na rafiki wa taifa la Israel, Lindsey Graham, ambaye alikuwa mmoja wa marafiki wakubwa zaidi ambao Israel imewahi kuwa nao. Hivyo hana budi kwenda kuwawakilisha raia wa Israel.

Mkutano wa pili kati ya Zelensky na Trump

Kwa upande wake Zelensky anatarajiwa kukutana na Trump katika Ikulu ya White House, kabla ya mazishi ya Seneta Graham. Huu utakuwa mkutano wao wa pili katika mwezi huu wa Julai.

Kabla ya mkutano huo, Zelensky ameonya kuwa Urusi imekuwa ikiisaidia Iran wakati vita vikiendelea kwa kunasa picha za satelaiti za vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko katika eneo la Ghuba, ambazo baadaye huonekana zikiwa mikononi mwa Iran.

Türk amesema Israel imeyashambulia maeneo yenye watu wengi LebanonPicha: Jung Yeon-je/AFP

Rais huyo wa Ukraine, pia amedai kwamba kulikuwa na ''uhusiano wa moja kwa moja'' kati ya picha zilizopatikana kutoka kwa Urusi na mashambulizi yaliyotekelezwa na Iran.

Jana, Trump alipuuza athari zozote zinazoweza kutokea kutokana na msaada unaodaiwa kutolewa na Urusi kwa Iran. Trump alisema hadhani kama wamekuwa wakifanya hivyo, na ikiwa ndivyo, basi athari zake zimekuwa ndogo sana au hazijaonekana kabisa. Hata hivyo, alisema kwamba atalizungumzia suala hilo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

UN: Israel yakiukaji sheria za kimataifa za kibinadamu

Katika hatua nyingine, Trump amesema kuna fursa nzuri za kupiga hatua katika mazungumzo na Iran, huku pande hizo mbili hasimu zikiendelea kujizuia kushambuliana kwa siku ya tatu mfululizo. Trump amesema ana matumaini kwamba juhudi mpya za kidiplomasia zinaweza kuhitimisha vita vilivyozuka mwishoni mwa mwezi Februari.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, amesema kuwa ofisi yake imerekodi ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu uliofanywa na Israel nchini Lebanon, na kwamba vitendo hivyo vinaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW