Netanyahu ziarani barani Afrika
4 Julai 2016Ziara yake hiyo ina mwelekeo wa kutafuta washirika wapya wa kibiashara pamoja na kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 40 ya tukio la kuwaokoa mateka nchini Uganda ambapo ndugu yake aliuwawa.
Katika taarifa muda mfupi kabla ya kuondoka kutoka Israel, Netanyahu aliitaja ziara hiyo ya kwanza kufanywa na waziri mkuu wa Israel katika eneo hilo baada ya kupita muda wa miongo kadhaa, kuwa ni ya "kihistoria".
Anatarajiwa kutuwa nchini Uganda mchana huu majira ya saa saba kwa saa za Afrika mashariki.
Ziara hiyo inakuja katika wakati ambapo Israel imeanzisha mpango wa misaada wenye thamani ya dola milioni 13 kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na ushirikiano na mataifa ya Afrika, imesema ofisi ya waziri mkuu Netanyahu.
Mapambano dhidi ya ugaidi
Israel pia itatoa kwa mataifa ya Afrika mafunzo katika "ulinzi wa ndani" na afya, taarifa hiyo imesema.
Baada ya Uganda , Netanyahu atakwenda Kenya, Ethiopia na Rwanda, lakini anatarajiwa pia kukutana na viongozi wengine wa Afrika katika mkutano nchini Uganda.
Netanyahu amesema katika taarifa kwamba "kuja katika ziara kama hii pia ni muhimu kwa mtazamo wa kidiplomasia, kiuchumi na kiusalama na ninafuraha kwamba Israel inarejea katika bara la Afrika kwa kiwango kikubwa, na kuongeza kwamba, "tunaifungua Afrika kuingia tena Israel."
Mzozo wa mataifa ya Kiarabu na Israel ulifungua mwanya kati ya mataifa ya Afrika na taifa hilo la Kiyahudi katika miaka ya 1960. Kufuatia vita kati ya Israel na majirani zake mwaka 1967 na 1973, mataifa ya Afrika kaskazini yakiongozwa na Misri yaliweka mbinyo kwa mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kuvunja mahusiano na Israel, ambapo mengi yalifanya hivyo.
Mahusiano hayakusaidiwa pia na urafiki wa Israel na utawala wa kibaguzi nchini Afrika kusini kabla ya utawala huo kuanguka mwaka 1994.
Katika mahojiano na gazeti la Uganda la Monitor kabla ya ziara hiyo, Netanyahu alisema ziara yake ni juhudi za kurejesha uhusiano.
"Niko wazi kuhusu hilo, ni kweli," Netanyahu alisema, kwa mujibu wa gazeti hilo.
Mateka wa Air France
Mbali na masuala ya kidiplomasia na biashara, ziara hiyo itakuwa na maana ya ndani ya kibinafsi kwa Netanyahu.
Kaka yake Yonatan aliuwawa Julai 1976 wakati akiongoza kikosi cha makomandoo kilichovamia uwanja wa ndege wa Entebe, nchini Uganda, kuwaokoa abiria waliokuwamo katika ndege ya shirika la ndege la Ufaransa Air France iliyotekwa nyara na Wapalestina wawili na Wajerumani wawili.
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Uganda Henry Okello Oryem aliliambia shirika la habari la AFP , kwamba Netanyahu atapokelewa kwa heshima ya mizinga 19 wakati atakapowasili , kabla ya kwenda katika tukio la kumbukumbu ya miaka 40 tangu kuokolewa kwa abiria hao tukio litakalofanyika katika eneo la uwanja wa zamani wa ndege.
Baadaye atahudhuria mkutano wa kupambana na ugaidi pamoja na viongozi wa Ethiopia, Kenya , Malawi , Rwanda, Sudan kusini na Zambia, kabla ya kwenda Kenya baadaye leo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga