Netanyahu ziarani Marekani kuijadili Iran
11 Februari 2026
Hii ni ziara ya sita kwa waziri huyo mkuu wa Israel nchini Marekani tangu kurejea kwa Trump katika Ikulu ya White House mwaka mmoja uliopita. Netanyahu na Trump walikutana pia mnamo Oktoba mwaka uliopita wakati Trump alipotangaza kusitisha mapigano huko Gaza.
Mkutano huu unakuja siku chache baada ya ule uliowakutanisha wanadiploamsia wakuu wa Iran na Marekani nchini Oman, ambapo Trump alisema duru nyingine ya mazungumzo baina yao itafuata katika siku zijazo lakini bila kueleza mahali na tarehe kamili ya mkutano huo.
Netanyahu na Trump wanakutana huku kukiwa na ukosoaji wa kimataifa unaozidi kuongezeko kuhusu hatua za Israeli za kuimarisha udhibiti wake katika eneo la Palestina inalolikalia kimabavu la Ukingo wa Magharibi.Itakumbukwa kwamba siku chache zilizopita, Baraza la mawaziri la usalama la Israel liliidhinisha hatua mpya zinazolenga kuimarisha udhibiti wa Israeli katika eneo hilo la kipalestina.
Hata hivyo, bado haijulikani wazi ikiwa suala hili litaibuliwa katika mazungumzo yao ya leo, licha ya hapo awali Trump kuonyesha wazi upinzani wake kuhusu hatua hizo za Israel katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi.
Ofisi ya Netanyahu ilisema mkutano huu sio tu kwamba utaangazia mpango wa nyuklia waIran lakini pia utagusia wasiwasi wao kuhusu silaha za makombora za Iran .
Israel imeongeza katika taarifa kwamba lazima makubaliano hayo yaijumuishe Iran kupunguza mipango yake ya makombora na kuacha kuyasaidia makundi ya wanamgambo kama ya Hamas na Hezbollah.
Iran yaonya kuhusu ziara hiyo
Hadi sasa, Iran imekataa kupanua wigo wa mazungumzo yake na Marekani zaidi ya suala la nyuklia, ingawa Washington pia inataka mipango ya makombora ya balistiki ya Iran na uungaji mkono wake kwa makundi ya wanamgambo iwe mezani.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran alionya hapo jana kwamba ziara hii ya Netanyahu itakuwa na ushawishi "mbaya" kwenye diplomasia na inaweza kuwa na athari mbaya katika eneo hilo la mashariki ya kati.
Wasiwasi wa Israeli uliongezeka zaidi wakati wa vita vya siku 12 kati yao na Iran mwaka uliopita na tangu wakati huo, maafisa wa Israeli wameonya mara kadhaa kwamba uwezo wa makombora wa Iran ni tishio kwa usalama wake.
Wakati wa vita hivyo, Iran ilirusha kwa mfululizo makombora ya balistiki na makombora mengine katika eneo la Israeli, na kushambulia maeneo ya kijeshi, ya kiraia na kufanya uharibifu mkubwa.
Marekani baadaye ilijiunga katika mashambulizi hayo kwa upande wa Israel na kushambulia maeneo matatu ya nyuklia ya Iran, kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Trump kuanza kutumika.