NEW DELHI: Rais wa Mexico Felipe Calderon azuru India
10 Septemba 2007Rais wa Mexico, Felipe Calderon, anaanza ziara rasmi ya siku mbili nchini India hii leo. Wizara ya mambo ya kigeni ya India imesema ziara ya rais Calderon huenda ikaimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya India na Mexico.
Rais Felipe Caldron amepangiwa kukutana na waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, na viongozi wengine wa kisiasa kujadili njia za kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili, ushirikiano wa kikanda na maswala ya kimataifa.
Viongozi hao wawili wanatarajiwa kutia saini mkataba wa ushirikiano katika kesi za uhalifu na kuzuia kutoza kodi mara mbili.
Rais Felipe Calderon, ambaye pia atakutana na viongozi wa kibiashara mjini New Delhi, ameandamana na viongozi zaidi ya 100 wa kibiashara.
Mexico na India ni nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi ambazo uchumi wao umekuwa ukikua kwa haraka katika miaka ya hivi karibuni, lakini biashara kati ya nchi hizo imekuwa ndogo.