NEW YORK: Annan aomba msaada zaidi kwa Pakistan
21 Oktoba 2005
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan ameomba msaada zaidi kwa eneo la kaskazini la Pakistan lililopigwa na tetemeko la ardhi.Amesema misaada zaidi inahitajiwa ili kuzuia wimbi la pili la vifo kutokana na magonjwa,njaa na baridi.Hesabu rasmi ya watu waliofariki katika tetemeko la ardhi inakaribia 50,000,lakini hakuna anaejua ni watu wangapi waliopoteza maisha yao katika sehemu za mbali ambako ni vigumu kwenda na hakuna wasaidizi walioweza kufika katika sehemu hizo.Mratibu wa misaada ya dharura ya Umoja wa Mataifa,Jan Egeland amelihimiza Shirika la Kujihami la nchi za Magharibi-NATO kuanzisha misafara ya kupeleka misaada kwa kiasi ya watu milioni 3 waliopoteza maskani zao katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan.Amesema misafara hiyo ya misaada ifanywe kabla ya kuanza kwa majira ya baridi kali.