NEW YORK: Annan kuongea na Bremer juu ya Iraq
19 Januari 2004Matangazo
Mratibu Mkuu wa shughuli za Marekani nchini Iraq, Paul BREMER anakutana baadaye leo mjini New York na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi ANNAN kujadiliana jinsi ya kuondoa tafauti kati ya pande hizo 2 kuhusu hali ya baadaye ya Iraq. Duru za Umoja wa Mataifa zimetaja kuwa Bwana ANNAN anakusudia kutumia mazungumzo hayo kwa kujaribu kuibinya zaidi Marekani ili ikubali kuushirikisha Umoja wa Mataifa katika taratibu za kuweka nguzo mpya ya maongozi nchini Iraq. Katibu Mkuu ANNAN, ambae ameomba kikao hicho ili apate uhakikisho kuhusu majukumu ya baadae ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq, atakutana pia katika mazungumzo hayo na Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Jeremy GREENSTOCK pamoja na ujumbe wa serikali ya mpito ya Iraq iliyowekwa na Marekani.