NEW YORK: Annan kusaidia kupata uhuru wa mateka wa Kiisraeli
5 Septemba 2006Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan amesema yupo tayari kuwa mpatanishi kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah,ili kusaidia kupata uhuru wa wanajeshi 2 wa Kiisraeli wanaozuiliwa na Hezbollah.Kwa mujibu wa msemaji wa Annan,pande hizo mbili zilitoa ombi hilo.Hayo yametokea wakati Annan alikuwa akikutana na viongozi wa Saudi Arabia mjini Jeddah.Wakati wa ziara yake ya Mashariki ya Kati Annan anataka azimio la Umoja wa Mataifa lililomaliza mapigano kati ya Israel na Hezbollah,liungwe mkono.Hapo awali alipokuwa Qatar,alisema mgogoro wa Iran kuhusu mradi wake wa kinuklia unapaswa kusuluhishwa kwa njia ya majadiliano.Siku ya Jumapili,rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran alimuambia Annan kuwa Teheran haitositisha harakati zake za kinuklia,lakini ipo tayari kufanya mazungumzo zaidi.