NEW YORK: Baraza la usalama lagawanyika juu ya Lebanon
7 Agosti 2006Mabalozi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamegawanyika juu ya azimio linalonuia kumaliza vita baina ya Israel na kundi la Hezbollah kusini mwa Lebanon.
Baraza la usalama lilikutana kujadili hatua ya Lebanon kulikataa azimio lililopendekezwa na Marekani na Ufaransa, ikisema azimio hilo haliitishi usitishwaji wa mapigano haraka.
Lebanon inataka wanajeshi wa Israel waondoke kusini mwa Lebanon mara moja. Wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wameshindwa kufikia makubaliano juu ya takwa hilo la Lebanon, katika kikao chao cha dakika tisini, wakiwa hawajui ikiwa walijumulishe sharti la Lebanon katika azimio hilo.
Azimio hilo litapigiwa kura hapo kesho na wala sio leo kama ilivyokuwa imepangwa.
Rais wa Syria, Bashar al Assad, amemwambia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kwa njia ya simu kwamba uamuzi wowote utakaochukuliwa bila Lebanon kukubali, utavuruga juhudi za kutafuta suluhisho na kuuzidisha mgogoro wa Mashariki ya Kati.