New York: Baraza la Usalama linajadili namna ya kujirekebisha, kimfumo
12 Julai 2005Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa imeanza kufanya majadiliano juu ya pendekezo la kulipanua baraza la usalama la umoja huo kutoka wanachama 15 wa sasa na kuwa 25. Moja kati ya miswaada ya maazimio iliowasilishwa unaweza ukazifanya Ujerumani, Japan, Brazil na India, kundi la nchi G nne, pamoja na nchi mbili za Kiafrika, kuwa wanachama wa kudumu wa baraza hilo. Viti vingine vinne vipya vitakuwa kwa wanachama wasiokuwa wa kudumu. Ili mswaada huo upitishwe, unahitaji kuungwa mkono na thuluthi mbili kati ya wanachama 191 wa Hadhara Kuu. Mswaada huo uliowasilishwa rasmi na balozi wa Brazil unakabiliana na upinzani mkubwa. Wapinzani ni pamoja na Algeria, Argentina na Pakistan. Mablozi wa nchi hizo wanasema majadiliano ya kulirekebisha baraza la Usalama yametekwa nyara na kikundi kidogo cha nchi ambazo zinajitakia nafasi mpya. Balozi wa Brazil amesema kikundi cha nchi hizo nne kitatafuta suluhisho na Umoja wa Afrika, AU.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, B ibi Condoleezza Rice, analiunga mkono takwa la Japan la kuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Akiwa ziarani huko Tokyo, Bibi Rice, alijizuwia kusema chochote kuhusu pendekezo la nchi hizo nne.