NEW YORK : G4 kuendelea kuzungumza na AU kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa
18 Julai 2005Brazil, Ujerumani,India na Japani zimekamilisha mazungumzo na ujumbe wa Umoja wa Afrika AU hapo jana na kukubali kuendelea na mazungumzo hayo kuondosha tafauti zilizobaki juu ya njia bora za kupata uwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa manne G4 Celso Amorim wa Brazil,Yoschka Fischer wa Ujerumani,Natwar Singh wa India na Nobutaka Machimura wa Japani walikutana katika mazungumzo ya chakula cha mchana na ujumbe wa watu 18 ulioongozwa na Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria Olu Adeniji ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.
Ujumbe wa AU pia unamjumuisha waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini Dlamini Zuma,Waziri wa masuala ya Afrika wa Libya Ali Triki na naibu waziri wa mambo ya nje wa Misri Samih Chukri kadhalika na maafisa waandamizi wengine 14 wa nchi wanachama wa umoja huo.
Nchi za kundi la G4 linaona kuungwa mkono na kundi la Afrika kwenye Umoja wa Mataifa ni muhimu kufanikisha kupitishwa kwa rasimu ya azimio lao juu kutanuka kwa Baraza la Usalama.
Pendekezo hilo linalopingwa na Marekani,Pakistan na Canada linakusudia kuongeza wanachama wa baraza hilo kutoka 15 wa hivi sasa hadi kuwa 25.