NEW YORK: Korea ya Kaskazini huenda ikawekewa vikwazo
14 Oktoba 2006Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamia kuweka vikwazo vya silaha na fedha dhidi ya Korea ya Kaskazini kwa sababu ya jaribio lake la kinuklia lililoripotiwa.Upelelezi uliofanywa na Marekani umethibitisha kuwa jaribio hilo lilitekelezwa.Inatarajiwa kuwa upigaji kura huenda ukachelewa kwa saa chache kwa sababu Urussi na China zimewasilisha mabadiliko katika mswada wa azimio,ambao ulitayarishwa na Marekani. Balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa,John Bolton amesema ana hakika kuwa azimio hilo litapitishwa leo hii.Siku ya Ijumaa,afisa wa Kimarekani alisema,uchambuzi uliofanywa na wapelelezi wa Kimarekani umeonyesha harakatiredio katika sampuli za hewa iliyokusanywa karibu na eneo linaloshukiwa kuwa ni mahala panapofanywa majeribio ya kinuklia ya Korea ya Kaskazini. Sampuli hizo zilikusanywa siku tano baada ya Pyongyang kutangaza kuwa imefanya jaribio hilo.Mswada mpya wa azimio sasa unaeleza wazi wazi kuwa matumizi ya kijeshi kuambatana na sura ya 7 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa si miongoni mwa hatua za kuchukuliwa.