1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Ujerumani yalipongeza azimio la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran

1 Agosti 2006

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio dhidi ya mpango wa kinyuklia wa Iran. Ujerumani imelikaribisha azimio hilo linaloipa Iran hadi tarehe 31 mwezi huu kusitisha shughuli zake zote za kurutubisha madini ya uranium la sivyo iwekewe vikwazo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema katika taarifa yake kwamba sasa ni jukumu la Iran kuzingatia hofu ya jumuiya ya kimataifa juu ya mpango wa kinyuklia.

Azimio la 1696 la baraza la usalama linaeleza wasiwasi mkubwa juu ya hatua ya Iran kukataa kutii amri ya shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, kukomesha urutubishaji wa madini ya uranium na shughuli nyengine za kinyuklia.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Javad Zarif, amelikataa azimio hilo.

Akizungumzia kuhusu azimio hilo, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Bolton, amesema,´Tunatumai azimio hili litaidhihirishia Iran kwamba njia muafaka ya kumaliza kutengwa na jumuiya ya kimataifa ni kuachilia mbali mpango wake wa kutaka kutengeneza silaha za kinyuklia. Tunatazamia Iran italitii azimio hili kikamilifu mara moja na bila masharti.´

Marekani na Umoja wa Ulaya zinahofu kwamba Iran huenda inataka kutengeneza silaha za kinyuklia. Rais Gerge W Bush wa Marekani amelipongeza azimio hilo. Qatar ni nchi mwanachama pekee wa baraza la usalama iliyolipinga azimio hilo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW