NEW YORK-Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani afanya ziara ya Marekani
28 Novemba 2005Kinachoangaliwa zaidi katika ziara hiyo ya waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ni uimarishaji wa uhusiano baina ya Ujerumani na Marekani,uliozorota kufuatia hatua ya Ujerumani kukataa kuiunga mkono Marekani katika vita vya Iraq.Lakini kingine kitakachochukua nafasi,ni juu ya ripoti za hivi karibuni za kuwepo ndege za shirika la ujasusi la Marekani CIA kutua katika nchi za Ulaya zikiwa zimewachukuwa watuhumiwa wa ugaidi na kuwapeleka katika jela za siri.
Akiwa mjini New York leo,Bwana Frank-Walter Steinmeier amepangiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.Viongozi hao wawili watajadiliana mchango wa Ujerumani katika kuufanyia mageuzi Umoja wa Mataifa na tamaa ya Berlin ya kuwa mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kesho Waziri Steinmeier ataelekea Washington kukutana na wawakilishi wa ikulu ya Marekani-White House,akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje,Condoleezza Rice na Mshauri wa masuala ya usalama Stephen Hadley.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani anatazamiwa kuwaeleza wenyeji wake juu ya makusudio ya serikali ya muungano ya Berlin kuimarisha mahusiano na Marekani baada ya kipindi cha kuzorota uhusiano huo baada ya Marekani na nchi washirika kuivamia Iraq.
Waziri Steinmeier ataweka bayana msimamo wa nchi yake kutopeleka vikosi vyake nchini Iraq au kujiingiza katika hatua yoyote ya kutoa mafunzo ndani ya nchi hiyo.Msimamo wa Ujerumani ni kwamba mafunzo kwa askari polisi wa Iraq na maofisa wa jeshi la nchi hiyo yataendeshwa nje ya Iraq.
Mbali ya masuala yatakayohusu mchakato wa ujenzi wa Iraq baada ya vita,Steinmeier atawajibika kushughulikia suala jengine tete.
Itakumbukwa hivi karibuni Ujerumani iliungana na kelele za karibu nchi nyingi za Ulaya,zinazochunguza ndege za CIA kusafirisha watuhumiwa wa ugaidi katika jela za siri,ambako vitendo vya utesaji vimekuwa vikitendeka.
Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na televisheni ya Ujerumani,zaidi ya safari 80 za ndege za CIA zilitua nchini Ujerumani pekee zikiwa njiani kuelekea katika mahabusu hizo za siri.
Kiongozi mwandamizi wa chama cha Christian Democrat,Wolfgang Bosbach ana matumaini kuwa suala hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi wakati wa ziara ya Bwana Steinmeier mjini Washington.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier,amesema atawajibika kutetea hoja zake kwa kutumia ukweli uliopo na sio kama alivyosoma katika magazeti.Wachunguzi wa masuala ya kisiasa,wanaamini suala hilo halitakuwemo katika taarifa rasmi wakati wa ziara hiyo,lakini hapana shaka litaelezwa hapo kesho atakapokutana na Bibi Condoleezza Rice.