NEW YORK.Mawaziri wa mambo ya nje wajadili mpango wa kikosi cha kulinda amani
16 Agosti 2006Kufuatia siku mbili tangu kupitishwa azimio la kusimamisha vita baina ya Israel na wapiganaji wa Hezbola nchini Lebanon, juhudi za kidplomasia zinaendelezwa kufanikisha azimio hilo la baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Uturuki, Pakistan na Malaysia wamekutana mjini Beirut kujadili mpango wa kuwapeleka wanajeshi wa kimataifa wa kulinda amani kusini mwa Lebanon.
Kwa upande mwingine wanadiplomasia wa nchi za umoja wa ulaya wanatarjiwa kukutana mjini Brussels, Ubelgiji kujadili mpango huo wa amani. Umoja wa mataifa unatarajia kuwapeleka wanajeshi wake 3,500 wa kulinda amani katika muda wa wiki mbili zijazo.
Wanajeshi hao watasaidia kuimarisha hatua ya kumaliza mapigano, kuondoka wanajeshi wa Israel na kuyawezesha majeshi ya Lebanon kuingia kusini mwa nchi hiyo.
Ufaransa, Uturuki na Malaysia zimesema ziko tayari kuwapeleka wanajeshi wake katika kikosi cha kulinda amani cha kimataifa nchini Lebanon.
Makamu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Hedi Annabi amesema kikosi cha askari wa kimataifa nchini Lebanon kitaongezeka hadi kufikia askari 15,000.