1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand yawazuia wanadiplomasia wa Urusi

29 Machi 2018

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Arden amesema Alhamisi hii kwamba nchi yake haitawaruhusu wanadiplomasia wa Urusi waliofukuzwa kwenye mataifa mengine kuingia nchini mwake.

Die neuseeländische Premierministerin Jacinda Ardern
Picha: picture-alliance/dpa/D.Munoz

Waziri mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden amesema hii leo kwamba nchi yake haitawaruhusu wanadiplomasia wa Urusi waliofukuzwa kwenye mataifa mengine kuingia nchini mwake, ikiwa ni hatua za kujibu shambulizi la sumu inayoua mishipa ya fahamu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi nchini Uingereza. Uingereza inaituhumu Urusi kufanya shambulizi hilo. 

Jaribio la mauaji dhidi ya jasusi huyo Sergei Skripal, ambaye ni kanali wa zamani wa kikosi cha ujaasusi katika jeshi la Urusi aliyewasaliti majasusi wengi wa Urusi kwa kutoa taarifa za kijaasusi kwa idara ya kijaasusi ya Uingereza, MI6, limepelekea kushusha mahusiano ya Urusi na mataifa ya magharibi na kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu enzi ya vita baridi. 

Baada ya Uingereza kuwafukuza wanadiplomasia 23 wa Urusi, ambayo iliwataja kama ni majasusi waliofanya shughuli zao chini ya mwamvuli wa kidiploamasia, Urusi ilijibu hatua hiyo kwa kuwafukuza pia wanadiplomasia 23 wa Uingereza. Marekani na mataifa mengine ya magharibi, ambayo ni pamoja na wanachama wengi wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO pia yaliwafukuza zaidi ya wanadiplomasia 100 wa Urusi.

New Zealand haijamfukuza raia yoyote wa Urusi, baada ya waziri mkuu Arden kusema hapo awali kwamba hakukua na majasusi wa Urusi katika ubalozi wa nchi hiyo ulioko New Zealand ambao serikali yake ingefaa kuwafukuza, tofauti na hali ilivyo kwa washirika wenzake katika masuala ya ujasusi.

Baadhi ya wanadiplomasia wa Urusi wakiondoka kwenye ubalozi ulioko London, UingerezaPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Augstein

Amesema hii leo kwamba angewaomba washirika wake kuwapa majina ya wanadiplomasia wa Urusi waliofukuzwa kutoka kwenye nchi hizo na hawatawaruhusu kuingia nchini mwake kupinga kile alichokitaja kama "hatua zisizofaa zinazochukuliwa dhidi ya Urusi" kufuatia shambulizi hilo la Uingereza.

Urusi kuomba msaada wa kisheria Uingereza katika kuchunguza shambulizi hilo.

Waziri Mkuu Arden amesema kwenye taarifa yake na hapa namnukuu "majina hayo hatimaye yataingizwa kwenye orodha ya zuio la kusafiri ili kuhakikisha kwamba watu binafsi waliobainika kufanya shughuli zinazokwenda kinyume na hadhi yao ya wanadiplomasia hawaruhusiwi kuingia New Zealand" mwisho wa kumnukuu.

Mjini Moscow, Svetlana Pentreko ambaye ni msemaji wa tume ya uchunguzi kuhusu shambulizi hilo ambalo pia lilimuhusisha binti ya Skripal, Yulia Skripal, amesema Urusi imetuma ombi kwa wenzake wa Uingereza la kuwasaidia kisheria kwa kuchukua hatua kadhaa zinazolenga kubaini mazingira ya uhalifu huo pamoja na kuwapatia nakala za vifaa vya uchunguzi wa makosa ya uhalifu.

Baadhi ya wanasiasa hapo awali walimkosoa waziri mkuu Ardern kwa kutochukua hatua kali dhidi ya Urusi, kwa kusema hatua hiyo inahatarisha mahusiano na washirika wake wa magharibi.

Profesa wa chuo kikuu cha Victoria anayehusika na masomo kuhusu usalama kilichopo mjini Wellington Robert Ayson amesema, mtizamo uliopo ni kwamba hatua zilizochukuliwa awali hazikuonyesha uthabiti wa kutosha na kwa maana hiyo wanajaribu hivi sasa kujirekebisha.

Naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje Winston Peters ameliambia bunge hapo jana kwamba shughuli nyingi za kijasusi zinazofanywa na majasusi wa Urusi dhidi ya New Zealand, hufanywa kutokea nje ya mipaka yake. 

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE

Mhariri:Yusuf Saumu