1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Neymar ajiunga na Al Hilal ya Saudi Arabia

16 Agosti 2023

Mchezaji wa klabu ya Paris Saint Germain Neymar amekamilisha uhamisho kujiunga na timu ya Al Hilal ya Saudi Arabia. Taarifa zinasema PSG itapokea kitita cha euro milioni 90.

Frankreich Neymar Jr.
Picha: Jean Catuffe/DPPI media/picture alliance

Neymar amekamilisha uhamisho kuelekea ligi ya nchini Saudi Arabia, Saudi Pro League, baada ya klabu ya Al Hilal kukubali kulipa kitita cha euro milioni 90 kwa timu ya Paris Saint Germain Jumatatu.

Kiwango hicho kitakuwa ni rekodi kwa ligi hiyo inayounhwa mkono na kudhaminiwa na dola hilo lenye utajiri mkubwa mafuta, katika mfululizo wa matumizi makubwa ya fedha kuwanunua wachezaji wenye vipaji vya kutandaza soka.

Al Hilal huenda hatimaye ikafanikiwa kumpata Neymar ili kukifikia kiwango cha Al Nassr, mahasimu wao wa mjini Riyadh, klabu ambayo ilimshawishi Cristiano Ronaldo kujiunga nayo mnamo Januari mwaka huu.

Ofa za hivi karibuni kwa Lionel Messi na Kylian Mbappè, wachezaji wa Neymar msimu uliopita katika klabu ya PSG, hazikukubaliwa. Inaripitiwa Neymar amepewa mkataba wa miaka miwili unaotarajiwa kumlipa mchezaji huyo nyota wa Brazil mwenye umri wa miaka 31, mshahara wa kasi dola milioni 100 kwa mwaka. Kiwango hicho kitakuwa ni takriban nusu ya mshahara anaolipwa Ronaldo mwenye umri wa miaka 38.

Wiki iliyopita Neymar na klabu ya PSG walikubaliana angeweza kuondoka ingawa, alivyotaka yeye, kama ilivyokuwa kwa Messi wiki kadhaa zilizopita, ilikuwa kurejea katika klabu yake ya zamani ya Barcelona. Masaibu ya kifedha yanaoikabili Barcelona yanaifanya mikataba kama hii kuwa migumu kuafikiwa na Messi badala yake alichagua kujiunga na Inter Miami katika ligi ya Marekani mnamo mwezi Juni.

Al Hilal ni mojawapo ya vilabu vinne vya Saudia vilivyotaifishwa kupitia Fuko la uwekezaji la Umma, PIF, ambalo lina mali ya thamani ya dola bilioni 700. Miongoni mwa mali hizo ni mashindano ya mchezo wa gofu ya LIV Golf ambayo yameipa changamoto mashindano ya kimataifa ya mchezo wa gofu ya PGA Tour kabla mashirika hayo mawili kukubaliana kushirikiana.

Fuko la PIF linaongozwa na mwanamfale wa Saudia Mohammed bin Salman kama mwenyekiti, ambaye nia yake katika michezo ya kimataifa imekuwa kitambulisho cha sera yake.

Usajili wa Neymar ulisonga mbele siku ambayo Al Hilal, washindi mara 18 wa ligi ya taifa, ilifungua msimu na mechi yake ya kwanza. Al Hilal ilicheza na Abha huku winga raia wa Brazil Malcom na kiungo wa Ureno Rúben Neves, ambao waligharimu kima cha juu kabisa cha fedha kama gharama ya uhamisho kuwahi kulipwa na klabu ya Saudi Arabia. Uhamisho wa Malcom uligharimu euro milioni 65 kutokea klabu ya Zenit Petersburg na Rúben Neves euro milioni 60 kutoka Wolverhampton.

(ape)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW