Neymar atambulishwa rasmi Ufaransa
7 Agosti 2017Msimu wa ligi nchini Ufaransa League 1 umefunguliwa rasmi mwishoni mwa Juma ambapo katika siku ya ufunguzi rasmi wa ligi hiyo siku ya Ijumaa Monaco mabingwa watetezi walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Toulouse na Jumamosi Paris St. Germain iliikandika Amiens kwa mabao 2-0 bila ya nyota wao Neymar waliyemnyakua hivi karibuni kutoka FC Barcelona ya Uhispania kwa kitita cha juu kabisa cha euro milioni 222. Hata hivyo kufunguliwa kwa ligi hiyo hakukuwa kwa kishindo kuliko PSG kumsajili nyota huyo kutoka Brazil , Neymar. Kocha wa PSG Unai Emery alisema , PSG ni timu kubwa bila ya Neymar, lakini Neymar anaiongezea umaarufu .
"Bila Neymar , PSG ni klabu kubwa lakini pamoja na Neymar inakuwa kidogo bora zaidi, kidogo kubwa zaidi na pia kuna njia tunaweza kumjumuisha mchezaji kama yeye, na pia kwa wengine ambao ni wachezaji wazuri, tunaweza kupiga hatua, tunaweza kuwa timu kubwa na pia ni kweli kwamba kwa msisimko wa mashabiki, muktadha ni mzuri, ni hali nzuri kabisa."
Mchezaji huyo ambaye donge la kumsajili la euro milioni 222 kutoka Barcelona limefikia rekodi ya dunia ya uhamisho , amezuiwa kucheza mchezo wake wa kwanza katika msimu mpya kwa kuwa usajili wake umemalizika kwa kuchelewa. Hata hivyo alitambulishwa kwa mashabiki wa timu hiyo katika uwanja wa parc des Princes mjini Paris kabla ya mchezo huo kuanza.
Nani kuchukua nafasi ya Neymah Barcelona ????
Swali na tetesi na minong'ono iliyomo katika vyombo vya habari kwa hivi sasa ni juu ya , nani anachukua nafasi ya Neymar katika Barcelona. Kuna majina kadhaa yanayotajwa ambapo mazungumzo yanaendelea na maafisa wa timu za wachezaji hao, ambapo jina linalotajwa sana ni Ousnane Dembele wa Borussia Dortmund kijana wa miaka 19 kutoka Ufaransa kuweza kuchukua nafasi hiyo adimu katika kikosi cha Barcelona. Pia yupo Philip Courtinho wa Liverpool , Mbrazil ambaye Barca wameweka kitita cha milioni 132 kumtwaa mshambuliaji huyo. Ni kipi kitakachotokea katika siku na wiki za kuelekea mwishoni mwa kufungwa kwa dirisha la usajili mwezi huu ni swali na kusubiri na kuona.
Kocha wa Manchester Jose Mourinho anaweza kunyakua taji moja la Ulaya ambalo bado hajawahi kulipata , wakati kikosi chake kitakapokutana na Real Madrid katika kombe la UEFA Super Cup kesho Jumanne katika mchezo wake wa kwanza kupambana na vigogo hao wa Uhispania tangu kutengana nao mwaka 2013.
Mourinho , ambaye timu yake ilishinda kombe la ligi ya Ulaya Europa League msimu uliopita na kuokoa kile ambacho huenda ni msimu wa kwanza uliokatisha tamaa chini ya kocha huyo kutoka Ureno, aliiongoza Real Madrid kupata ubingwa wa La Liga kwa kutia kibindoni pointi 100 ikiwa ni rekodi na kushinda kombe la mfalme katika kipindi kati ya mwaka 2010 hadi 2013.
Mafanikio yake hayo hata hayo hata hivyo katika Santiago Bernabeu waligubikwa , na kukosana na wachezaji muhimu katika kikosi hicho kama Sergio Ramos na Iker Casillas pamoja na migongano na marefa na wapinzani pamoja na kushindwa kunyakua kombe la Champions League, wakati Real iliposhindwa katika nusu fainali kila mwaka.
Mwandishi: Sekione Kitojo/dpae,afpe,rtre,ape
Mhariri: Mohammed Khelef