Mkutano wa G20 umefikia malengo licha ya mivutano
23 Novemba 2025
Mkutano wa kilele wa siku mbili wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi duniani la G20 unaomalizika Jumapili jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, umetoa ishara ya uthabiti. Michael Sheldrick wa Global Citizen amesema: "Licha ya mivutano katika siasa za kilimwengu, mkutano huu wa kilele wa G20 umeonyesha kuwa ushirikiano wa kimataifa bado unawezekana ikiwa nchi zitawajibika."
Urais wa kupokezana wa G20 unaoshikiliwa kwa sasa na Afrika Kusini umefanikiwa kuhamasisha muungano mpana ili kuharakisha upanuzi wa nishati mbadala barani Afrika, alisema Sheldrick. Takriban watu milioni 600 barani Afrika wanaishi bila umeme. Washiriki walipitisha kwa kauli moja tamko la mwisho baada ya mazungumzo kugubikwa na mpango wa amani wa Marekani kuhusu mzozo wa Ukraine huku Washington yenyewe ikiususia mkutano huo.
Mzozo wa Ukraine wagubika mazungumzo ya G20
Mpango wa Marekani wa kukomesha vita nchini Ukraine uligubika mazungumzo katika mkutano huo wa G20 . Kyiv, washirika wake wa Ulaya na hata baadhi ya wabunge wa Marekani wanaupinga mpango huo. Marekani imesema ipo nafasi ya kuujadili tena kabla ya mazungumzo ya Jumapili kuhusu pendekezo hilo yatakayofanyika nchini Uswisi.
Trump ameipa Ukraine hadi Novemba 27 kuidhinisha mpango huo wa kukomesha vita vya karibu miaka minne, lakini Kyiv inataka kufanyike mabadiliko kwenye rasimu hiyo ambayo inaafiki baadhi ya matakwa ya Urusi yenye msimamo mkali. Siku ya Jumamosi, Washington ilisisitiza kwamba pendekezo hilo ni sera rasmi ya Marekani, ikikanusha madai yaliyotolewa na kundi la maseneta wa Marekani wakidai kwamba Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio aliwaambia kuwa rasimu hiyo ilikuwa na "upendeleo" kwa Urusi.
Mpango huo wenye vipengee 28 unaitaka Ukraine, nchi iliyovamiwa kuachilia baadhi ya maeneo yaliyonyakuliwa kinyume cha sheria, kupunguza ukubwa wa jeshi lake hadi zaidi ya nusu na kuahidi kuwa kamwe haitojiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Hata hivyo rais wa Marekani Donald Trump amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumamosi kwamba hilo halikuwa pendekezo lake la mwisho na anatumai kusitisha mapigano "kwa njia moja au nyingine". Mjumbe maalum wa Trump kwa Ukraine, Keith Kellogg amesema mpango huo "unaendelea kuboreshwa."
Mataifa ya Ulaya ambayo ni washirika wakuu wa Ukraine baada ya Marekani, hawakushirikishwa katika kuandaa pendekezo hilo, wamesema wakati wa mkutano huo wa G20 kuwa mpango huo unahitaji "kazi ya ziada" huku wakitoa mapendekezo ya kuimarisha maslahi ya Kyiv.
Mkutano wa Geneva kulijadili pendekezo hilo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mrekani Marco Rubio na mjumbe maalum wa Trump Steve Witkoff wamewasili mjini Geneva-Uswisi siku ya Jumapili kushiriki mazungumzo hayo na kwamba Mkuu wa Jeshi la Marekani Daniel Driscoll tayari amewasili Geneva baada ya kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.
"Pendekezo la amani lililoandikwa na Marekani, limetolewa kama nguzo imara ya mazungumzo yanayoendelea. Linategemea mchango kutoka upande wa Urusi. Lakini pia linategemea mchango wa awali na unaoendelea kutoka Ukraine, aliandika Rubio kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi jioni.
Wawakilishi wa Urusi na Ukraine wanatarajiwa pia kuhudhuria mazungumzo hayo. Zelensky aliteua ujumbe wake unaongozwa na msaidizi wake mkuu Andriy Yermak. Zelensky amesema "mashauriano yatafanyika na washirika wote kuhusu hatua zinazohitajika ili kukomesha vita", ingawa hakukuwepo uthibitisho wa Moscow kushiriki katika mazungumzo hayo.
Zelensky amesisitiza kuwa wawakilishi wake wanajua namna ya kuyatetea maslahi ya kitaifa ya Ukraine na hatua zinazohitajika ili kuizuia Urusi kuanzisha uvamizi mwingine wa tatu, baada ya kulinyakua eneo la rasi ya Crimea mwaka wa 2014 na kuanzisha uvamizi kamili mnamo mwaka 2022.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema maafisa watakutana Geneva "ili kuendeleza majadiliano zaidi", akisisitiza umuhimu wa "hakikisho thabiti la usalama" kwa Ukraine katika makubaliano yoyote.
Starmer amesema mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa, Jonathan Powell, atashiriki mazungumzo ya Geneva. Vyanzo vya kidiplomasia vya Italia vimesema Roma imemtuma mshauri wa usalama wa taifa Fabrizio Saggio, na kwamba maafisa wa usalama kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Ufaransa na Ujerumani pia watahudhuria.
Viongozi wakutana kando ya mkutano huo wa G20
Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wamefanya mazungumzo kuhusu vita vinavyoendelea nchini Ukraine, hali katika Ukanda wa Gaza, ushirikiano katika sekta ya ulinzi, madini, nishati safi na akili mnemba.
Viongozi hao wawili wamekutana kando ya mkutano wa kilele wa G20 uliofanyika Afrika Kusini , unaofanyika nchini Afrika Kusini na wamethibitisha tena uungaji mkono kwa Ukraine na kusisitiza kwamba, makubaliano yoyote ya amani ni lazima yaihusishe Kyiv moja kwa moja, yalinde maslahi yake ya msingi na yajumuishe hakikisho thabiti za usalama.
Kuhusu Gaza, Carney na Merz wameelezea kuunga mkono mpango jumla wa amani wenye lengo la kukomesha vita na kuwezesha misaada ya kibinadamu kuingia kwa wingi katika ardhi hiyo ya Wapalestina.
Msimamo thabiti wa mataifa ya Ulaya
Katika taarifa yao ya pamoja, mataifa ya Ulaya yakishirikiana na Canada na Japan yamesema kuwa mpango wowote wa amani unatakiwa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa. Wakizungumza pembezoni mwa mkutano huo wa kilele wa G20 nchini Afrika Kusini, wamesema mpango wa Marekani ni "msingi ambao utahitaji kazi ya ziada", huku wakisisitiza kuhusu kanuni ya kwamba mipaka haipaswi kubadilishwa kwa kutumia mabavu huku wakielezea wasiwasi wao kuhusu pendekezo la kupunguzwa kwa jeshi la Ukraine, ambalo litapelekea nchi hiyo kuwa kwenye hatari ya kushambuliwa katika siku zijazo.
Macron amesema kuna vipengee katika mpango huo ambavyo vinapaswa kujadiliwa kwa mapana kwani vinayahusu pia mataifa ya Ulaya. Mambo hayo ni pamoja na uhusiano wa Ukraine na jumuiya ya NATO na mali zilizozuiwa za Urusi na zinazoshikiliwa katika Umoja wa Ulaya. "Sote tunataka amani na tunakubaliana kwa hilo. Tunataka mpango imarana wa kudumu wa amani na kwamba suluhu yoyote ni lazima izingatie usalama wa wakazi wote wa Ulaya, " alisisitiza rais Macron.
Ukraine yajikuta njia panda
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema katika hotuba yake kwa taifa siku ya Ijumaa kwamba Ukraine inakabiliwa na moja ya nyakati ngumu zaidi katika historia yake, akiongeza kwamba atapendekeza "njia mbadala" kwa mpango huo wa Trump.
" Hili ni moja wapo la shinikizo kubwa zaidi kwa Ukraine: Tunakabiliwa na chaguo gumu sana: kupoteza heshima yetu au hatari ya kumpoteza mshirika muhimu," Zelensky alisema, akimaanisha uwezekano wa kutengana na Washington.
Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa upande wake amesema mpango huo unaweza "kuwa msingi" wa suluhisho la mwisho la amani, lakini akatishia kunyakua ardhi zaidi ikiwa Ukraine itajiondoa kwenye mchakato huo wa mazungumzo.
// RTR/AFP/AP/DPA