1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni ipi kazi ya Polisi wa maadili wa Iran?

27 Septemba 2022

Kifo cha Mahsa Amini, ambaye alikamatwa kwa madai ya kutovaa hijabu yake ipasavyo, kimewaweka "polisi wa maadili" wa Iran chini ya uangalizi mkubwa. Lakini je, polisi hao ni akina nani na shughuli yao haswa ni ipi?

Iran, Teheran | Proteste nach dem Tod von Mahsa Amini
Picha: WANA NEWS AGENCY/REUTERS

Wanaoitwa polisi wa maadili nchini Iran walimkamata Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 huko Tehran kwa kosa la kuvaa "mavazi yasiyofaa" na kumpeleka kwenye kituo cha polisi, ambapo alipoteza fahamu. Siku tatu baadaye, alikufa akiwa hospitalini.

Kifo chake kimezua hasira na kusababisha maandamano makubwa dhidi ya serikali ambayo yanaendelea kuripotiwa katika miji kadhaa, kulingana na video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii. Serikali ya Rais Ebrahim Raisi imetuma vikosi vya usalama, kukabiliana na waandamanaji.

Polisi wa IranPicha: picture-alliance/ dpa

Ni akina nani "polisi wa maadili" na ni vipi wanavyofanya kazi?

"Gasht-e-Ershad," ambayo hutafsiriwa kama "doria elekezi" na inayojulikana mno kama "polisi wa maadili," ni kitengo cha polisi cha Iran kilichopewa jukumu la kutekeleza sheria na kanuni za mavazi ya Kiislamu pindi watu wakiwa hadharani.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, wanawake wote walio katika umri wa kuweza kuolewa lazima wavae nguo zenye stara na wafunike nywele zao kwa mtandio au hijab ingawa umri halisi haujafafanuliwa wazi. Shuleni, wasichana kwa kawaida hulazimika kuvaa hijabu kuanzia umri wa miaka 7, lakini hiyo haimaanishi kuwa wanalazimika kuivaa katika maeneo mengine ya umma.

Polisi wa Iran akiandaa kutekeleza hukumu ya kunyongwa hadharani kwa watu wawili waliokutwa na kosa la mauaji mwaka 2007 huko Tehran.Picha: Abedin Taherkenareh/EPA/picture-alliance/dpa

Iran na sheria ya Kiislamu

Sehemu kubwa ya kanuni za kijamii za Iran zinatokana na tafsiri ya sheria ya Kiislamu, ambayo inawataka wanaume na wanawake kuvaa kwa heshima. Hata hivyo, kiutendaji, "polisi wa maadili" kimsingi huwalenga zaidi wanawake.

Hakuna miongozo au maelezo yaliyo wazi juu ya aina gani za nguo zisizostahili au zisizofaa, na hivyo kila mtu kuwa na tafsiri yake binafsi na kuzua shutuma kwamba watekelezaji wa "sheria za maadili" huwazuia wanawake kiholela.

Soma zaidi:Raia wa Iran waendelea kuandamana licha ya onyo la Mahakama 

Wale wanaozuiliwa na "polisi wa maadili" hupewa notisi au, wakati mwingine, hupelekwa kwenye kile kinachoitwa kituo cha elimu na ushauri au kituo cha polisi, ambapo wanatakiwa kuhudhuria mhadhara wa lazima juu ya hijabu na maadili ya Kiislamu. Kisha wanapaswa kumwita mtu wa kuwaletea "nguo zinazofaa" ili waweze kuachiliwa huru.

Mahsa Amini(22) aliyefariki baada ya kushikiliwa na Polisi wa maadili nchini IranPicha: Social Networks/ZUMA/picture alliance

Polisi hao husimamia pia utekelezaji wa kanuni za mavazi

Mbali na kukabiliana na ukiukaji wa hijab, serikali inaendeleza mafunzo ya kanuni za mavazi ya Kiislamu mashuleni, kwenye vyombo vya habari vya kitaifa na hata kwenye matukio ya umma.

Hata hivyo, wanawake wengi wa Iran wamebuni njia za kukaidi kanuni za mavazi za kihafidhina. Wengi wamechupa mipaka kwa kuvaa nguo zinazobana na kutumia hijabu zenye rangi huku nywele nyingi zikionekana wazi, hasa ikiwa hakuna sheria iliyo wazi juu ya kiasi gani cha nywele kinachoweza kudhihirika au laa.

Utafiti wa mwaka 2018 uliochapishwa na Bunge la Iran ulionyesha kuwa kati ya asilimia 60 hadi 70 ya wanawake wa Iran hawafuati kanuni za "mavazi ya Kiislamu" haswa wakiwa hadharani.

Soma zaidi: Watu 31 wauawa kwenye maandamano nchini Iran

Kwa miongo kadhaa, wanaharakati wamekuwa wakipambana dhidi ya hijab ya lazima na baadhi yao wako gerezani kwa sasa. Chini ya utawala wa Ebrahim Raisi ambaye ni mhafidhina, "polisi wa maadili" wamezidisha uwepo wao katika miji mikubwa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, maelfu ya wanawake walianza kwenda barabarani bila hijabu na wengine walionekana hivyo katika video mitandaoni ili kuwatia moyo wengine kufanya hivyo.

Waandamanaji nchini Canada wanyoa nywele zao ili kupinga kifo cha Mahsa Amin (pichani).Picha: Mert Alper Dervis /AA/picture alliance

Polisi wa maadili wapingwa nchini Iran na kwengineko

Baada ya video ya mwanamke akimsihi afisa wa "polisi wa maadili" kumuachilia binti yake mgonjwa kusambaa mitandaoni mnamo mwezi Julai, wito ulikua wa kufutwa kwa maafisa hao.

Soma zaidi: Raisi aonya waandamanaji nchini Iran

Katika hali ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa nchini Iran, mamia ya wanawake wenye msimamo wa kidini walianza kudhihirisha upinzani wao dhidi ya hijabu ya lazima mtandaoni.

Hata baadhi ya watu wenye misimamo ya kihafidhina wakiwemo wabunge walianza kuikosoa sheria na jeshi la polisi wakisema kuwa imekuwa na athari mbaya kwa mitazamo ya umma kuhusu vazi la hijabu na dini kwa ujumla.

(DW-English)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW