1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Vita vya Gaza vinavyounganisha Uturuki na Misri

4 Septemba 2024

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekuwa akimtaja Rais wa Misri kama "muuaji", lakini sasa anatumia neno "ndugu". Mabadiliko haya ya karibuni yamechochewa na mitizamo inayofanana juu ya vita kati ya Israel na Hamas.

Türkei |  Treffen ägyptischer Präsident Abdel Fattah al-Sisi mit  Recep Tayyip Erdogan in Ankara
Picha: Murad Sezer/REUTERS

Kama hii leo ingekuwa ni mwaka 2019, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wala asingefikiria mara mbili kukutana na Abdel Fattah el-Sissi wa Misri.

Kwa mtizamo wake, el-Sissi alikuwa "ni muuaji."

Lakini nyakati za maneno makali zimekwisha. Na Jumatano hii El Sissi alikaribishwa mjini Ankara kwa mara ya kwanza kabisa.

"Ndugu badala ya muuaji"

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ulidorora mwaka 2013, baada ya Rais wa Misri aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohammed Morsi wa kundi la Udugu wa Kiislamu kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa wakati huo, Abdel-Fattah el-Sissi, ambaye hatimaye alichaguliwa kuwa rais mwaka 2014.

Itikadi ya Udugu wa Kiislamu linaloungwa mkono na Uturuki, imechangia katika uundwaji wa sera za Erdogan. Mara nyingi ametumia ishara ya mkono ya kundi hilo tangu kuanza kwa maandamano makubwa yaliyomuondoa Morsi mwaka 2013.

Soma pia:Maoni: Wamisri hawana cha kuchagua

Tetemeko la ardhi nchini Uturuki ni moja ya matukio yaliyoashiria kurejea kwa uhusiano kati ya Uturuki na Misri, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri kuzuru eneo lililoathirikaPicha: Pierre Verdy/dpa/picture alliance

Lakini baadae, mahusiano yakaanza kunawiri. Marais wote wawili walikivunja kihunzi kwa kupeana mikono wakati wa Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar. Hii ilifuatiwa na hatua za kurekebisha zaidi maelewano ya kidiplomasia, baada ya tetemeko kubwa la ardhi nchini Uturuki mnamo 2023.

Siku chache baada ya tetemeko, El-Sissi alimpigia simu Erdogan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Samih Shoukry alizuru eneo lililoathiriwa. Viongozi hawa  walikutana tena mwaka 2023, kwenye mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 tajiri kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi duniani, G20 nchini India.

Mwezi Februari, el-Sissi alimkaribisha Erdogan mjini Cairo, huku wote wakionyesha furaha kubwa. Na kuanzia hapo, Erdogan akaanza kutumia neno "ndugu yangu mpendwa", badala ya "muuaji" ya mwaka 2019.

Israel inahusikaje?

Tangu kuzuka kwa vita huko Gaza, "Misri imekuwa muhimu zaidi kwa Uturuki," anasema Selin Nasi, mchambuzi wa kisiasa katika Shule ya Uchumi ya London, alipozungumza na DW, na kuongeza kuwa licha ya uhusiano wa Uturukina Israeli kuzidi kuzorota, Misri iimekuwa lango kuu la kuingiza misaada Gaza.


Lakini, misimamo inayofanana ya nchi hizo mbili kuhusu mzozo wa Israel na Palestina inahisiwa kuchochea maelewano baina yao. "Nchi zote mbili zinaunga mkono haki halali ya Wapalestina ya kuwa na taifa huru na zina wasiwasi wa juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Gaza," alisema Nasi.

Rais wa uturuki Recep Tayyip Erdogan(kushoto) akisalimiana na Abdel Fattah el-Sissi wa Misri alipotembelea taifa hilo Februari 2024Picha: Turkish Presidency/AP/dpa/picture alliance

Gamal Abdel Gawad, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Marekani chenye makao yake mjini Cairo, ameiambia DW kwamba mataifa hayo yanasimama pamoja kuhusu utatuzi wa mzozo wa Gaza na ushirikiano wao pia utarahisisha kufikia malengo yao katika eneo hilo.

Manufaa ya pande zote kiuchumi

Balozi wa zamani wa Uturuki nchini Qatar Mithat Rende, yeye ameiambia DW kwamba hata uchumi wa nchi hizo mbili unategemeana kwa kuwa Misri ina utajiri wa nishati na Uturuki ina miundombinu imara ya viwanda. Akasema "Wawekezaji wa Uturuki wanavutiwa sana na Misri".

Manowari iliyobeba nafaka chini ya makubaliano ya kusafirisha nafaka katikati ya mzozo kati ya Urusi na Ukraine ikipita kwenye eneo la Bosphorus mjini Istanbul, Uturuki July 15,Picha: MEHMET CALISKAN/REUTERS

Selin Nasi anakubaliana na Balozi Rende na kuongeza kuwa Misri imezidi kuibuka kama kiungo muhimu katika suala la nishati" na Uturuki inataka kufaidika na hili.

"Habari njema"

Waangalizi wanaona kupunguzwa kwa mivutano kati ya nchi hizo mbili kutaleta maendeleo mazuri na matokeo yatakayovuka eneo hilo.

Nchi hizo mbili zinadhibiti sehemu muhimu ya biashara ya kimataifa, amesema Balozi Rende, akiangazia Mlango wa Bahari wa asili na ujia muhimu kimataifa wa maji uliopo Istanbul, Uturuki, maarufu "Bosphorus Dardanelles pamoja na Mfereji wa Suez.

Akasema, ulimwengu uko katika wakati ambapo minyororo ya ugavi inasambaratika na siku moja, ushindani kati ya Marekani na China unaweza kukua na kuwa mzozo.