1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni kwa nini Saudia na nchi nyingine zataka uanachama BRICS?

22 Agosti 2023

Baadhi wanaamini kuwa kundi hilo la BRICS linaweza kutumia ushawishi wake wa kisiasa na nguvu ya kiuchumi kuhimiza mageuzi yanayohitajika katika taasisi kama vile Benki ya Dunia.

BRICS pia inashinikiza kuundwa kwa sarafu ya pamoja katika jitihadi ya kupunguza utawala na utegemezi wa sarafu ya dola ya Marekani.
BRICS pia inashinikiza kuundwa kwa sarafu ya pamoja katika jitihadi ya kupunguza utawala na utegemezi wa sarafu ya dola ya Marekani.Picha: Li Tao/Xinhua/picture alliance

Kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani BRICS – Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini – litakutana kwa mkutano wa kila mwaka unaoanza leo mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Kutanuliwa kwa BRICS ni miongoni mwa ajenda kuu katika mkutano wa mwaka huu. Nchi 23 tayari zimetuma maombi rasmi ya kuwa wanachama wa kundi hilo, zikiwemo Saudi Arabia, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, Argentina, Indonesia, Misri na Ethiopia.

Mkutano wa kilele wa mwaka huu hasa umepata umaarufu kutokana na matarajio kwamba kundi hilo la BRICS linaweza kutanuka kwa kuongeza wanachama wapya wakati Urusi na China zikijaribu kuongeza ushawishi wao wa kisiasa katikati ya ongezeko la mvutano kati yao na Marekani pamoja na washirika wake.

Kundi la BRICS lilianzaje?

Ilianza kwa kifupi kama BRIC, neno lililobuniwa mwaka 2001 na mchumi Jim O'Neill katika benki ya uwezekaji ya Marekani ya Goldman Sachs, ili kuunganisha pamoja uchumi wa nchi nne kubwa na zinazokuwa kwa kasi zaidi wakati huo.

Rais Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini haiwezi kulazimishwa kuchukuwa upande katika mizozo ya kimataifa.

O'Neil alisisitiza kuwa uchumi wa mataifa manne – Brazil, Urusi, India na China – kwa pamoja nchi hizo zina uwezo wa kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi duniani katika muda wa muongo mmoja ujao.

Picha: BRICS/AA/picture alliance

Wawekezaji na watunga sera kwenye mataifa hayo walikumbatia wazo la mchumi Jim O'Neil. Wakiweka kando tofauti zao za kisiasa na kijamii, nchi hizo zinazoendelea zilihisi kufungamanishwa na msukumo wa pamoja wa kurekebisha mifumo ya kisiasa na kifedha ya kimataifa inayoongozwa na Marekani.

Lengo lao kuu ni kuwa na mifumo iliyo ya "haki, uwiano na uwakilishi sawa.”

Viongozi wa BRIC walifanya mkutano wao wa kwanza wa kila mwaka mnamo mwaka 2009 mjini Yekaterinburg, Urusi. Mwaka mmoja baadae, waliialika Afrika Kusini kujiunga na kundi hilo, na baada ya hapo neno "S" likaongezwa kwenye BRIC, na ndio maana hadi leo kundi hilo linafahamika kama BRICS.

Umuhimu wake ni upi?

Wanachama wa BRICS wanawakilisha zaidi ya asilimia 42 ya idadi jumla ya watu duniani na wanachangia karibu robo ya pato la taifa la kimataifa pamoja na asilimia 18 ya biashara duniani kote.

Rais wa Indonesia kuhudhuria mkutano wa BRICS Afrika Kusini

Kundi hilo linachukuliwa kama mbadala wa taasisi za kiuchumi na kisiasa za mataifa ya Magharibi kama vile G7 na Benki ya Dunia.

Rais wa China Xi Jinping alikuwa mwenyeji wa mkutano wa 14 wa kilele wa Jumuiya ya BRICS Juni 23, 2022.Picha: Li Xueren/Xinhua/IMAGO

Baadhi wanaamini kuwa kundi hilo la BRICS linaweza kutumia ushawishi wake wa kisiasa na nguvu ya kiuchumi kuhimiza mageuzi yanayohitajika katika taasisi kama vile Benki ya Dunia na Shirika la fedha la kimataifa IMF kwenda sambamba na hali halisi ya jinsi ulimwengu ulivyo kwa wakati huu.

Je, BRICS imepata mafanikio gani hadi sasa?

BRICS imejitahidi sana kufikia malengo yake ya kuwa mbadala wa mifumo ya jadi ya kifedha na kisiasa.

Miongoni mwa mafanikio yake, ni kuanzishwa kwa benki mpya ya maendeleo ama kwa kifupi benki ya BRICS, ambayo ni benki ya maendeleo ya kimataifa yenye mtaji wa dola za Kimarekani bilioni 50 ili kufadhili miundombinu na miradi inayohusiana na masuala ya tabianchi katika nchi zinazoendelea.

Hali yatulia: Afrika Kusini yakwepa kumkamata Putin

Benki hiyo, inayojumuisha wanachama wa BRICS ikiwa ni pamoja na Bangladesh, Misri, na Umoja wa Falme za Kiarabu kama wanahisa wake, hadi sasa imeidhinisha mikopo ya zaidi ya dola bilioni 30 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2015. Hata hivyo kwa upande wa Benki ya Dunia, taasisi hiyo ya fedha ilitoa zaidi ya dola bilioni 100 mwaka 2022 pekee.

BRICS pia imeunda mpango wa akiba ya dharura wa dola bilioni 100, akiba ambayo inaweza kutumiwa na nchi wanachama panapotokea msukosuko wa kifedha duniani.

Xi Jinping awasili Afrika Kusini

00:45

This browser does not support the video element.

Sarafu ya pamoja

BRICS pia inashinikiza kuundwa kwa sarafu ya pamoja katika jitihadi ya kupunguza utawala na utegemezi wa sarafu ya dola ya Marekani.

Hata hivyo, sarafu ya BRICS haitarajiwi kuundwa hivi karibuni. Kutokana na hilo, kundi hilo limelekeza nguvu zake katika kuimarisha matumizi ya fedha za ndani wakati wa kufanya miamala ya kibiashara kati ya wanachama.

Mchumi Jim O'Neil katika chapisho lake la maoni mwaka 2021, alisema na hapa namnukuu, "Kando na kuunda benki ya BRICS, ni vigumu kuona mafanikio mengine yaliyopatikana kando na mikutano yao ya kila mwaka.”

Mafanikio machache ya BRICS yanaweza kuelezewa na maslahi yanayotofautiana miongoni mwa wanachama wake, hasa China na India, ambazo zinazozana juu ya mpaka wa McMahon na kushuhudia kudorora kwa uhusiano kati yao katika miaka ya hivi karibuni.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW