1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yapiga marufuku utoaji habari kuhusu mapambano

26 Novemba 2021

Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atayeandika habari kuhusu harakati za kijeshi kwenye mapambano ya vikosi vya serikali na TPLF nchini Ethiopia wakati waziri mkuu Abiy Ahmed akiwaongoza wanajeshi wake vitani

Äthiopien I Tigray-Krise
Picha: AP/picture alliance

Serikali ya Ethiopia imetangaza sheria mpya inayokataza hatua ya utoaji taarifa kuhusu kinachoendelea kwenye uwanja wa mapambano katika vita vinavyoendelea kati ya vikosi vyake dhidi ya waasi wa Tigray.

Sheria hiyo mpya iliyotangazwa jana alhamisi inasema ni marufu kusambaza kwa njia yoyote ya mawasiliano shughuli za aina yoyote za kijeshi na yanayojitokeza kwenye uwanja wa mapambano,ikiwa hayajachapishwa rasmi na serikali.

Ikumbukwe kwamba serikali ya mjini Addis ilitangaza hali ya dharura nchi nzima mwanzoni mwa mwezi huu wakati ikielezwa kwamba wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF wanakaribia kuufikia mji mkuu huo,katika mapigano hayo yanayoshuhudiwa kwa kiasi mwaka sasa.

 Tahadhari imezidi kutolewa na Jumuiya ya Kimataifa kuhusu vita hivyo kuongezeka katika nchi hiyo ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika huku serikali za kigeni zikionesha kuwa na wasiwasi mkubwa na kuwatolea mwito raia wao waondoke nchini humo.

Picha: AP/picture alliance

 Kwa mujibu wa tamko la serikali linaloweka wazi kuhusu Amri iliyotolewa ni kwamba vikosi vya usalama vitachukua hatua zinazostahiki dhidi ya wale watakaokutwa wanakiuka amri hiyo. Kimsingi amri hiyo inawezekana ni onyo la moja kwa moja kwa  vyombo vya habari na wale wanaotumia mitandao ya kijamii ambao wamekuwa wakiripoti kuhusu madai yanayotolewa kutoka upande wa waasi ya kupiga hatua katika kuyadhibiti maeneo kadhaa.

Aidha serikali ya Ethiopia imewapiga marufuku wakaazi wake kutumia mitandao mbali mbali ya kijamii kuliunga mkono ama moja kwa moja au kwa njia zisizowazi kundi la TPLF ambalo imeliita ni kundi la kigaidi ,na kuonya juu ya kuchukuliwa hatua kali kwa watakaokwenda kinyume,ingawa hatua hizo hazikuwekwa wazi.

Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Kadhalika amri hiyo ya serikali pia inapiga marufuku mtu yoyote kutoa mwito wa kutaka iundwe serikali ya mpito ikiwa ni siku moja baada ya chama cha upinzani chenye uungwaji mkono mkubwa cha Oromo Federalist Congress OFC kutoa taarifa inayotowa mwito wa vita kumalizwa na kuundwa serikali ya mpito itakayoratibu mazungumzo ya kuleta maridhiano nchini humo.

Chama hicho siku ya Jumatano kilitoa tamko linalopendekeza kwamba kuundwe serikali ya muda na katika kipindi hicho vyama vyote vianze mazungumzo ya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mpito itakayowashirikisha watu wote ambayo itaiongoza nchi kwa muda wa miezi 18.

Aidha mnamo Jumatano pia kituo cha habari cha serikali kiliripoti kwamba Abiy Ahmed  aliyewahi kuwa luteni kanali wa jeshi alijiunga kwenye mstari wa mbele wa mapambano kwenye jimbo la kaskazini mashariki la Afar,kukiongoza kikosi cha wanajeshi wake kupambana kwenye vita hivyo,huku akiyakabidhi madaraka kwa naibu wake.

Kundi la TPLF linazidi kupata nguvu likiwa tayari limeshaingia kwenye mikoa jirani ya Amhara na Afar na wiki hii likidai kuuteka mji mmoja ulioko kilomita 220 kutoka Addis Ababa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW