1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni miaka 30 tangu kuanguka ukuta wa Berlin

9 Novemba 2019

Shamrashamra za maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin zimekwishaanza kote nchini Ujerumani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel asema "hakutakuwa na ukuta mrefu ama mpana sana ambao hautavunjwa."

Deutschland Berlin Gedenkfeier 30 Jahre Mauerfall Merkel
Picha: Reuters/F. Bensch

Wakuu wa mataifa ya Poland, Hungary, Slovakia na Jamhuri ya watu wa Czech wamehudhuria sherehe hizo kwenye mtaa wa Bernauer ambako sehemu iliyosalia ya ukuta huo ipo ambako waliweka maua ya waridi katika nyufa za ukuta ambao ulikuwa kizuizi cha kutisha kilichougawa mji wa Berlin kwa miaka 28.

Mkuu wa makumbusho ya ukuta huo Axel Klausmeier amezizungumzia picha za Waberlin waliokuwa na furaha kutoka Mashariki na Magharibi waliokuwa wakilia kwa furaha na kukumbatiana jioni ya Novemba 9, 1989.

Klausmeier alitoa heshima zake kwa waandamanaji wa maandamano hayo ya amani mashariki mwa Ujerumani pamoja na mataifa jirani ya mkataba wa Warsaw, ambao waliingia mitaani wakishinikiza uhuru na demokrasia, pamoja na mageuzi kwenye sera za aliyekuwa kiongozi wa Umoja wa Kisovieti, Mikhail Gorbachev.  

Maandamano hayo pamoja na msururu wa watu waliokimbia Ujerumani ya Mashariki kwa pamoja viliongeza shinikizo kwa serikali ya kikomunisti kufungua mipaka yake kwa watu wa magharibi, hatua ambayo pia ilisababisha kuhitimishwa kwa mgawanyiko wa baada ya vita.

Miaka 30 baadaye, Ujerumani imekuwa taifa lenye nguvu kubwa zaidi kiuchumi pamoja na kisiasa, lakini bado kukiwa na masuala miongoni mwa watu wa Ujerumani kuhusu namna taifa hilo lilivyosimamia mabadiliko kutoka ujamaa hadi ubepari.

Meya wa Istanbul aonya kuhusu migawanyiko ya kisiasa.

Kuvunjwa kwa ukuta wa Berlin mnamo Novemba 9 mwaka 1989 kulifuatia uasi wa amani kwenye iliyokuwa Ujerumani Mashariki baada ya kuimarika kwa vuguvuvu miongoni mwa mataifa ya Ulaya yaliyokuwa kwenye eneo linalodhibitiwa na uliokuwa muungano wa kisovieti, walioamua kuzigeuzia mgongo siasa za Moscow.

Baadhi ya rai wakitembelea eneo la ukuta lililosalia ambalo liliwekwa maua kwenye maadhimisho hayo.Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Karibu matukio 200 yamefanyika katika kipindi cha wiki moja iliyopita ikiwa ni pamoja na kuoneshwa kwa vidio ya wakati maelfu ya raia wa Ujerumani mashariki walipouvunja ukuta huo uliokuwa na urefu wa kilometa 155 ili kuingia upande wa magharibi.

Meya wa Istanbul na kiongozi wa upinzani nchini Uturuki Ekrem Imamoglu alipozungumza na DW kwenye maadhimisho hayo ameonya dhidi ya migawanyiko ya kisiasa.

"Kuta si lazima ziwe ni zile zinazoonekana," alisema wakati alipozuru Berlin kwa maadhimisho hayo. "Sio lazima ziwe zimejengwa kwa zege ama vipande vya chuma. mara nyingine, watu wawili wanaweza kusimama pande tofauti na ukuta unajitokeza katikati yao."

Mchana wa leo viongozi wa maeneo mbalimbali ya Ujerumani waliwasha mishumaa kwenye ukuta kunapofanyika kumbukumbu hizo kwenye mtaa wa Bernauer mjini Berlin, baada ya viongozi wakuu wa Ujerumani na wageni kutoka nje kutembelea eneo hilo. 

Kansela Angela Merkel alipozungumza na gazeti la Ujerumani la Süddeutsche, Merkel amesema huenda mchakato wa muungano kati ya Magharibi na Mashariki ukachukua hata miaka 50 hadi kukamilika.

Kulikuwa na tukio la kuwasha mishumaa kuadhimisha siku hiyo Picha: Reuters/F. Bensch

"Katika masuala kadhaa, ambako inaaminiwa kwamba kila kitu kinaweza kufanana kati ya Mashariki na Magharibi hii leo tunashuhudia kwamba inaweza kuchukua nusu muongo ama zaidi" aliliambia gazeti hilo la Süddeutsche.

Ni nyakati zinazoonyesha furaha na wasiwasi kihistoria.

Kansela Merkel aliyekulia Ujerumani mashariki aidha amesema akiwa kwenye kanisa la kihistoria kulikokuwa kukifanyika maridhiano kwamba hakuna aliyetarajia hilo lingewezekana. Anasema "nakumbuka wale waliouawa kwenye ukuta ule kwa sababu ya kupigania uhuru." 

Amesema Novemba 9 inaashiria "nyakati za wasiwasi na furaha katika historia", huku tarehe hiyo pia ikielezea baadhi ya kurasa mbaya za huko nyuma za Ujerumani.

Mapema hii leo rais Steinmeier kupitia tovuti yake aliwaalika raia wa Ujerumani kusimulia shuhuda zao binafsi za kuanguka kwa ukuta huo wa Berlin.

Rais wa Italia Sergio Matarella ameelezea tukio la kuanguka kwa ukuta huo wa Berlin kama "mwanzo wa uhuru na njia mpya ya historia ya Ujerumani, bara la Ulaya pamoja na ulimwengu mzima."

Matarella amesema, "Ulaya bila ya kuta ya utenganisho na bila ya chuki ni fursa kubwa kwa raia kuwa wasimamizi wa mustakabali wao wenyewe."

Hata hivyo maadhimisho ya mwaka huu yameonekana kuwa na mwamko hafifu kuliko yaliyopita kutokana na haya ya sasa kufanyika katika wakati ambapo kuna hali tete barani Ulaya kwa sehemu ikiwa ni matokeo ya kitisho kinachotokana na kuibuka kwa siasa kali za kizalendo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW