1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni miaka kumi tangu NATO kuiingilia Kosovo

24 Machi 2009

Ni miaka kumi tangu Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuishambulia Serbia bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuhusiana na jimbo la Kosovo.

Vikosi vya KFOR vikishika doria KosovoPicha: AP

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya marehemu rais Slobodan Milosevic kukataa kutia saini makubaliano ya amani yatakayowalazimu wanajeshi wake kusitisha vita dhidi ya wakazi wa Kosovo walio na asili ya Albania wanaotakakujitenga. Chini ya misingi ya sheria za kimataifa hatua hiyo bado haijafafanuliwa kinagaubaga.

Jumuiya ya Kujihami ya NATO iliamua kuingilia kati baada ya mazungumzo ya amani kuambulia patupu kwa lengo la kuzuia mauaji yaliyo na misingi ya kikabila.Hali hiyo ilikwisha dhihirika Croatia na Bosnia-Herzegovina.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya NATO kwa Katibu Mkuu wa wakati huo Javier Solana kuyaamuru majeshi yake kuingia katika eneo lisilokua lake.Kulingana na wakosoaji mataifa wanachama wa Jumuiya ya NATO yalikiuka sheria za kimataifa kwani Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halikuidhinisha hatua hiyo.Umoja wa Mataifa ulitaka vikosi hivyo viondoke kwenye eneo hilo vilevile mapigano kusitishwa.Kiongozi wa wakati huo Slobodan Milosevic alikataa katakata kuyaamuru majeshi yake kusitisha kampeni zao dhidi ya wapiganaji wanaotaka kujitenga wa Kosovo walio na asili ya Albania.Kwa upande mmoja kujiingiza huko kwa NATO kulikuwa kwa dharura kwa lengo la kuyaokoa maisha ya wengi na kudumisha amani.

Hilo lilihalalisha hatua hiyo na baada ya majuma machache yapata raia laki 8 walilazimika kuyakimbia makazi yao.Joseph Marko mtaalam wa sheria za kimataifa anaeleza kuwa sheria za kimataifa zina mapungufu .
''Suala la Kosovo lilizua mitazamo tofauti katika sheria za kimataifa.Ni dhahiri kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bado halijakuwa na mfumo maalum inapozuka hali kama hiyo kwasababu ya nchi wanachama zilizo na kura ya turufu.
Hatua ya NATO kuingilia kati kwasababu za kuzuia janga la kibinadamu ilichochea mabadiliko ya mtazamo katika suala la kuheshimu utawala wa nchi .Hii ni kwasababu haipaswi kuingilia masuala ya ndani ya nchi.''

Hata hivyo mtaalam huyo anaamini kuwa sheria za kimataifa hazipo bayana katika hali kama hiyo.Mjadala uliopo sasa ni ikiwa kuna umuhimu zaidi wa kuheshimu utawala na haki za nchi na wakati huohuo kuwajibika kuwalinda raia.
Kutokana na hilo mateso yaliyo na misingi ya kikabila au kidini yanaweza kuisababishia nchi kupoteza haki hiyo.Hali halisi inaashiria mengine.

Kulingana na Franz-Lothar Altmann mtaalam wa masuala ya eneo la Balkani kutoka mji wa Munich sheria za kimataifa wakati mwengine ni nduma kuwili.Anatolea mfano suala la Georgia wakati ambapo Urusi ilivamia jimbo la Ossetia Kusini.

''Urusi imekuwa ikiunga mkono suala la kuheshimu mipaka vilevile kutounga mkono harakati za kutaka kujitenga ila kilichotokea ni kwamba ilifanya kinyume ya hicho. ''

Kimsingi hilo halikubaliki hata katika misingi ya kuzuia janga la kibinadamu.
Linajitokeza hapa suala la mauaji ya halaiki ambalo mazingira yake bado hayajapata ufafanuzi kamili.Jee ni watu wangapi wanapaswa kuuawa kabla ya mauaji hayo kuelezwa kuwa ya halaiki?Kadhalika matukio ya Kosovo yanatofautiana na yale ya majimbo ya Georgia.


Mwandishi: Schmidt,Fabian ZR/Mwadzaya

Mhariri:Abdul-Rahman