Ni mwaka mmoja baada ya shambulizi la mjini Berlin
19 Desemba 2017Soko hilo maarufu la Krismasi lililoko katika eneo la Breitscheidpaltz mjini Berlin litafungwa hii leo kwa siku nzima ikiwa ni ishara ya heshima kwa wahanga wa shambulizi hilo lililofanywa na raia wa Tunisia ambaye maombi yake ya kupatiwa hifadhi nchini Ujerumani yaligonga mwamba.
Kumbukumbu hizo za mwaka mmoja za shambulizi zinafanyika siku moja baada ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kukutana na ndugu wa wahanga wa tukio hilo kwa mara ya kwanza ikiwa ni baada ya kukosolewa kwa kushindwa kukutana nao mapema.
Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir anatarajiwa kutoa hotuba kwenye kumbukumbu hiyo itakayofanyika katika kanisa lililopo eneo hilo itakayofuatiwa na uzinduzi wa mnara wa kumbukumbu wenye urefu wa mita 14 uliyopakwa rangi ya dhahabu na uliyoandikwa majina ya wahanga wa tukio hilo.
Jioni ya leo watu watapata nafasi kushiriki maombi hayo katika muda ule ule ambao Anis Amri aliendesha lori katika soko hilo la Krismasi lililokuwa limefurika watu ambapo pia kengele za kanisa zitalia kwa dakika 12.
Amri aliuawa kwa kupigwa risasi siku nne baada ya shambulizi hilo na polisi nchini Italia ambako aliwahi kuishi.
Kurt Beck afisa aliyepewa jukumu na serikali ya Ujerumani kufuatilia na kushughulikia madhara yaliyotokana na shambulizi hilo amekiri hapo jana Jumatatu kuwa Kansela Merkel alichelewa kukutana na familia za wahanga wa shambulizi hilo la mwaka jana.
Serikali yakiri mapungufu yaliyojitokeza baada ya shambulizi
Naye Kansela Merkel akizungumzia lawama hizo dhidi yake alikiri na kusema ni wazi kwamba machungu waliyo nayo ndugu wa wahanga wa shambulizi hilo la mwaka jana hayawezi kupoozwa kirahisi lakini hata hivyo watafanya kila watakaloweza kuboresha masuala yanayostahili kuboreshwa.
Jeshi la polisi nchini Ujerumani nalo pia limekosolewa baada ya kubainika kuwa Anis Amri aliyewasili nchini Ujerumani wakati wa majira ya kiangazi mwaka 2015 na kujisajili kwa utambulisho tofauti tofauti alipaswa kuwa amefukuzwa kabla ya kutekeleza shambulizi hilo.
Jumapili iliyopita gazeti la Welt am Sonntag nchini Ujerumani liliripoti kuwa Anis Amri alikuwa akifuatiliwa nyendo zake kwa karibu na majasusi wa Ujerumani tofauti na ilivyofikiriwa awali.
Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas naye pia amesema serikali ya Ujerumani haikuwa imejiandaa kiasi cha kutosha kwa athari zitakazowakumba wahanga wa mashambulizi ya aina hiyo na kuongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo serikali inachopaswa kufanya ni kuomba radhi.
Maas amependekeza kuanzishwa idara ya uratibu serikalini kwa ajili ya kushughulikia majanga kama hayo ili muhanga yeyote wa mashambulizi yanayoweza kutokea siku zijazo apate mara moja mtu wa kushughulikia masuala yake katika ngazi ya kiserikali. Aidha ametoa mwito wa sheria kufanyiwa marekebisho ili wahanga wote wa mashambulizi ya kigaidi wahudumiwe na kulipwa fidia sawa sawa bila kujali utaifa wao au silaha zilizotumika katika shambulizi.
Wakati huohuo watu wamekuwa bado wakiendelea kumiminika katika soko hilo la Krismasi ingawa kumbukumbu ya shambulizi hilo la mwaka jana bado zina gonga katika mioyo.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/DW
Mhariri: Iddi Ssessanga