Ni nani kati yao atakayewika mara hii?
30 Novemba 2012Messi mshambuliaji wa Barcelona mwenye umri wa miaka 25, tayari ameshinda mataji hayo mara tatu na MuArgentina huyo anapigiwa upatu kushinda tena tuzo hii ambayo itatangazwa mjini Zurich mnamo Januari saba baada ya kura kupigwa na waandishi habari, manahodha wa timu za taifa pamoja na makocha.
Kama atashinda, anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kushinda taji hilo mara nne, baada ya kujiunga na gwiji wa Ufaransa na rais wa sasa wa Shirikisho la Soka Ulaya UEFA Michel Platini kama wachezaji pekee kushinda mara tatu mfululizo. Nyota wa Uholanzi Johan Cruyff na Marco Van Basten pia wamewahi kushinda matatu.
Mkufunzi wa Uhispania Vicente del Bosque ambaye aliongoza timu yake kushinda taji la UEFA EURO 2012 na kuwa wa kwanza kushinda vinyang'anyiro vitatu mfululizo ni miongoni mwa wanaopigiwa upatu kutwaa tuzo ya kocha bora. Atapambana na Jose Mourinho wa Real Madrid na Pep Guardiola aliyekuwa wa Barcelona. Kwa upande wa tuzo ya mchezaji bora kwa wanawake, bingwa mara tano wa Brazil Marta atapambana na Wamarekani Aby Wambach na Alex Morgan.
El Classico ya ujerumani: Bayern na Dortmund
Viongozi wa Bundesliga, Bayern Munich wanalenga kuwapiga kumbo mabingwa Borussia Dortmund katika kinyang'anyiro cha kuwania taji la ligi kuu ya soka Ujerumani Bundesliga wakati miamba hao wawili watakutana Jumamosi hii. Bayern wako pointi 11 mbele ya Dortmund na tayari wana faida ya kuwa kileleni mwa ligi. Kama watashinda leo, Dortmund wanaweza vile vile kuyazika matumaini yao ya kupata kombe kwa mara ya tatu mfululizo hata kabla ya nusu ya msimu kufika. Baada ya misimu miwili bila ya taji, Bayern wameshinda 12 kati ya mechi zake 14 za ligi msimu huu na hawatelezi katika msimu huu wa baridi jinsi ilivyokuwa msimu uliopita.
Dortmund wamewashinda Bayern katika mechi zao nne za mwisho katika bundesliga na kuwakalifisha magoli matano kwa mawili katika mechi yao ya mwisho ambayo ilikuwa ni kombe la Shirikisho mwezi Mei mwaka jana. Kiungo wa Dortmund, Mario Gotze anasema bado ni mapema na chochozte kinaweza kutokea. Lakini naye Manuel Neuer mlinda lango wa Bayern anasema ni wakati wa kuwashinda Dprtmund tena. Bayern walimpumzisha kiungo Bastian Schweinsteiger dhidi ya Freiburg katikati ya wiki naye kocha wa Dortmund Jurgen Klopp akawapumzisha Goetze, Ilkay Guendogan na Mats Hummels. Bayern wanaongoza ligi na pointi 37 mbele ya Bayer Leverkusen ambao wana 27, Dortmund ni wa tatu na 26 Schalke, Eintracht Frankfurt wakifwata na 24 kila mmoja.
Leverkusen ambayo ndiyo timu ya pekee kuwapiku Bayern msimu huu inawaalika Nuremberg leo, nayo Schalke itachauana dhidi ya Borussia Moenchengladbach. Schlake wameshinda tu mara moja katika mechi zao tano za mwisho nayo Frankfurt nayo inaonekana kuisha kasi baada ya kupata ushindi mmoja tu katika mechi sita. Mechi nyingine za Jumamosi ni kati ya Mainz na Hanover, nao wanaoshikilia mkia Augsburg wapambane na Freiburg wakati Greuther Fuerth wakifunga kazi dhidi ya Stuttgart. Jumapili, Wolfsburg watawaalika SV Hamburg nao Hoffenheim wamenyane na Werder Bremen katika kile kinachoonekana kuwa ni lazima kocha wa Hoffenheim Markus Babbel ashinde au aonyeshwe mlango.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef