1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Nia ya Marekani kuichukua Greenland yaanza kuitafuna NATO

13 Januari 2026

Shinikizo kutokana na hoja ya Marekani kutumia nguvu za kijeshi kuitwaa Greenland kijeshi, limeiweka Jumuiya ya Kujihami ya NATO mahala pabaya kwani mikakati na sera zake zinajikita katika kupambana na adui aliyeko nje.

Greenland Nuuk 2025 | Ndege ikionekana kuukaribia mji mkuu
Ndege ndogo ya kibiashara ikiingia Nuuk, Greenland, mnamo Machi 11, 2025. Rais wa Marekani Donald Trump anaangazia ikiwemo hatua za kijeshi kuchukua udhibiti wa Greenland, Ikulu ya White House ilisema Januari 6, 2025, na kuongeza mvutano ambao Denmark inaonya unaweza kuuvuja muungano wa NATO.Picha: Odd Andersen/AFP

Kufikia sasa, Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte amekuwa akilinyamazia suala hilo ila mkakati huo hautaleta tija.

Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen ametahadharisha mwanzoni mwa wiki kuwa iwapo Marekani itaamua kuivamia kijeshi nchi mwanachama wa muungano huo wa kijeshi, kila kitu kitafikia kikomo. Kwa mantiki hiyo, Jumuiya na operesheni zake zote za usalama zilizozinduliwa mwishoni mwa Vita Vikuu ya Pili vya Dunia zitasitishwa.

Athari za vitisho na kauli hizo kwa NATO hazitakiwi kupuuzwa

Kwa mtazamo Patrick Oksanen, mchambuzi wa Shirika la Utafiti la Stockholm Free World Forum, hali iliyopo kwenye NATO kwa sasa ni ushindi kwa Urusi. Hii ni kwa sababu kauli na vitisho vinatolewa wakati ambapo umepita muda mfupi baada ya Marekani kuivamia Venezuela na pia mshauri wa rais Trump, Stephen Miller, kuhoji uhalali wa Denmark kuwa msimamizi wa Greenland na iwapo vikosi vyovyote vya bara la Ulaya vitaidhibiti Marekani.

Kulingana na Ed Arnold aliyezungumza na DW, kitendo cha Jumuiya hiyo kukaa kwenye meza ya mazungumzo kujadili kitisho kutoka kwa mmoja ya nchi wanachama kinatoa picha mbaya.

Kwa mtazamo wa baadhi ya wachambuzi, pendekezo moja ni washirika wa NATO kupeleka vikosi vyao Greenland, kumpa ishara Rais Trump kuwa suala la ulinzi wanalipa uzito mkubwa na kwamba hahitajiki kuchukua hatua hiyo.

Nembo ya NATO - OTAN inaonyeshwa kwenye simu ya mkononi na NATOPicha: Jonathan Raa/Sipa USA/picture alliance

Ulaya yaonywa juu ya usalama wa eneo la Arctic

Kwa upande wake, Steven Everts, mkurugenzi katika Taasisi ya Usalama ya Umoja wa Ulaya, mataifa ya Ulaya yanapaswa kulichukulia suala la usalama wa eneo la Arctic kwa uzito mkubwa na iwapo yapo mapungufu yaweze kufanyiwa kazi.

Mbunge wa Denmark katika Bunge la Umoja wa Ulaya Anders Vistisen, anaafiki mtazamo wa Steve Everts na kusisitiza kuwa ipo haja ya kuwa wakweli na kusitisha michezo ya kidiplomasia au kujaribu kuirai Marekani kutumia hekima na busara kadhalika kutenga hela zaidi kwa ulinzi wa kijeshi.

Kimsingi inachotaka Marekani hakiwezekani. Pendekezo jengine kutoka kwa wachambuzi wa Ulaya, ni kusitisha mkataba wa biashara kati ya Marekani na Ulaya ambao unatazamwa kuwa unaipendelea, hadi pale Washington itakapokomesha vitisho vya kutaka kuimiliki Greenland.

Kwenye kikao cha Paris cha kuiunga mkono Ukraine siku ya Jumanne, viongozi wa Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Uingereza wailiunga mkono taarifa ya Waziri Mkuu wa Denmark Frederiksen na kwa pamoja kusisitiza kuwa walio na wajibu wa kulifanyia kazi suala hilo ni Denmark na Greenland pekee.

Taarifa hiyo ilitolewa muda mfupi kabla ya kikao na wawakilishi wa Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner ambaye ni mkwe wa Rais Donald Trump, bila ya kuchelea athari ambazo zinaweza kutokea ukizingatia juhudi za Marekani za kuiunga mkono Ulaya kwenye suala zima la Ukraine.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW