NIAMEY:Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan aizuru Niamey nchi inayokabiliwa na ukosefu wa chakula.
24 Agosti 2005Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan yupo nchini Niger,kujionea hali halisi ya njaa iliyosababishwa na ukame ilivyoiathiri nchi hiyo,baada ya Umoja wa Mataifa kushutumiwa kutochukuwa hatua za kutosha za kupeleka misaada ya chakula.
Akiwa huko Bwana Annan atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Niger,Hama Amadou,juu ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kukabiliana na hali mbaya ya ukosefu wa chakula,iliyoikumba nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa nchi masikini sana duniani.
Bwana Annan akiongozana na mkewe,ametembelea kitengo cha hospitali inayowapatia tiba watoto waliothiriwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa chakula na pia kijiji chenye kituo maalum,kinachotoa lishe kinachoendeshwa na madaktari wasio na mipaka,ambao awali walidai kuwa chakula cha msaada kilichotolewa na Umoja wa Mataifa hakikuwa kinawafikia walengwa.
Leo Bwana Annan anakutana na Rais Mamadou Tandja wa Niger pamoja na maofisa wa serikali,kuzungumzia namna ya kusaidia zaidi maeneo yaliyoathiriwa vibaya na ukosefu wa chakula.