1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Maduro aapishwa rasmi kwa muhula wa tatu

10 Januari 2025

Rais wa Venezuela Nicholas Maduro ameapishwa Ijumaa kwa muhula wa tatu wa miaka sita. Hata hivyo hali ya wasiwasi imeendelea kutanda nchini huo kuelekea hafla hiyo.

Venezuela Caracas 2025 | Maduro akiapishwa
Rais Maduro akila kiapo cha uraisPicha: Jhonn Zerpa/Miraflores Palace/Handout/REUTERS

Nicholas Maduro amekuwa madarakani tangu mwaka 2013. Kuapishwa kwake kwa muhula wa tatukunajiri baada ya tume ya uchaguzi nchini mwake kumtangaza mshindi wa uchaguzi uliofanyika mwezi Julai. Ushindi ambao uliidhinishwa na mahakama ya juu zaidi nchini humo, licha ya upinzani na pia ukosoaji wa wachunguzi kimataifa.

Matokeo kamili ya kura hiyo hayajachapishwa rasmi. Lakini upinzani nchini Venezuela unasema takwimu za kura zinaonesha aliyekuwa mgombea wao, Edmundo Gonzalez, ambaye pia serikali nyingi  za Magharibi, ikiwemo Marekani, zinamtambua kama rais mteule, alishinda kwa kishindo.

Miezi kadhaa tangu uchaguzi huo, baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa upinzani pamoja na waandamanaji wamekamatwa. Gonzalez alikimbilia Uhispania, lakini ameahidi kurejea Venezuela kuchukua Madaraka.

Maandamano ya kumpinga MaduroPicha: Ariana Cubillos/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Venezuela imeushutumu upinzani na kusema unapanga njama za kifashishti dhidi yake. Serikali hiyo imesema itamkamata Gonzalez endapo atarejea nchini humo na ipetoa kima cha dola 100,000 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kumtia nguvuni.

Soma: Upinzani waapa kuchafua shughuli ya kuapishwa Maduro

Kuelekea kuapishwa kwa Maduro, serikali ya Venezuela imefunga mipaka na anga yake na Colombia kwa muda wa saa 72. Hayo yamesemwa na wizara ya mambo ya nje ya Colombia.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni amepinga kile alichokitaja kuwa ‘kurejea kusikokubalika kwa ukandamizaji' nchini Venezuela. Hii ni baada ya Maria Corina Machado, kiongozi wa upinzani, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda alipokuwa akiongoza mkutano unaompinga Maduro.

Soma kwa kina: Wasiwasi umetanda Venezuela kabla Maduro kuapishwa

Kwenye taarifa, Meloni amesema wanakusudia kuhakikisha kuna ukabidhiaji Madaraka wa amani na kidemokrasia na kwamba matumaini ya uhuru na demokrasia ya Wavenezuela ni sharti yatimizwe. Hata hivyo Meloni hakutaja hatua yoyote maalum.

Italia ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na pia mwanachama wa mataifa saba yaliyoinukia kiviwanda G7, hufuatilia kwa karibu matukio nchini Venezuela ambako raia wengi nchini humo ni wa asili ya Italia.

Maduro baada ya kuapishwaPicha: Matias Delacroix/AP Photo/picture alliance

Wapinzani wa serikali wameripoti wimbi jipya la matukio ya ukandamizajikuelekea uapisho wa Maduro. Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za ukamataji wa kiholela na vitisho dhidi ya wakosoaji wa serikali.

Mara nyingi kwenye utawala wake wa miaka 12 iliyopita na iliyojaa misukosuko, Maduro mwenye umri wa miaka 62, ameshutumiwa pakubwa. Lakini kwa ukaidi ameendelea kusalia Madaraka.

Soma: Mtu mmoja amekufa katika maandamano ya Venezuela

Mnamo mwaka 2018, Marekani ilimwekea vikwazo lakini kufuatia urafiki na usaidizi wa Urusi na China, aliweza kustahimili vikwazo hivyo vya kiuchumi.

Serikali ya Venezuela inachunguzwa na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC kwa makosa ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW