1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Yaunde

6 Februari 2015

Niger inapanga kutuma wanajeshi nchini Nigeria kujiunga na kikosi cha mataifa kadhaa kupambana na wanamgambo wa Boko Haram huku baraza la Usalama la Umoja wa mataifa likihimiza opereshini za kijeshi dhidi ya Boko Haram.

Ramani ya Nigeria inayoonyesha kule wanajeshi wa Chad walikoingia kupambana na boko Haram

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limezitolea wito nchi jirani na Nigeria ziimarishe opereshini za kijeshi na ushirikiano wa vikosi vyao vya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa Boko Haram.

Katika azimio lililopitishwa kwa sauti moja,nchi 15 wanachama wamezisihi nchi za eneo hilo ziimarishe opereshini zao na ushirikiano wa kimkoa ili kuweza kupambana vizuri zaidi na haraka dhidi ya Boko Haram.Kwa namna hiyo baraza la Usalama la Umoja wa mataifa "limesifu mkutano wa wataalam unaofanyika mjini Yaounde nchini Cameroon kwa lengo la kukamilisha mipango ya kuundwa na kutumwa wanajeshi 7500 wa kiafrika kupambana na Boko Haram.

Mkakati wa kupambana na Boko Haram wadurusiwa

Wataalam dazeni kadhaa wa kiafrika na ulaya wanahudhuria tangu jana mjini Yaounde,mkutano unaotajwa kuwa "muhimu" katika kutathmini mkakati wa mpambano dhidi ya Boko Haram.

Wanajeshi wa TchadPicha: AFP/Getty Images/M. Medina

"Mkutano huo wa siku tatu utapelekea kupitishwa uamuzi muhimu kujibu wito wa jumuia ya kimataifa kuimarisha juhudi za kupambana na Boko Haram" amesema waziri wa ulinzi wa Cameroon Alain Mebe Ngo'o.

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limesifu pia mchago wa Tchad katika kupambana na Boko Haram nchini Nigeria.

Wanajeshi wa Tchad wameanza hujuma za nchi kavu kutoka nchi jirani ya Cameroon,dhidi ya Boko Haram katika mji wa mpakani wa Gamboru nchini Nigeria.

Boko Haram wanadhibiti eneo kubwa kaskazini mashariki ya Nigeria na kutishia pia usalama wa nchi jirani.

Bunge la Niger litaamua jumtatu

Niger imeamua kujiunga na Cameroon inayopambana dhidi ya Boko Haram tangu miezi kadhaa sasa na Tchad iliyoteremka vitani tangu wiki chache zilizopita dhidi ya Boko Haram.

Raia wnaokimbia ukatili wa Boko Haram wakipita katika vituo vya ukaguzi wa polisiPicha: Reuters/Afolabi Sotunde

Bunge la Niger litapiga kura jumatatu ijayo kuhusu kutumwa wanajeshi hao wa Nigeria na kwa namna hiyo kufungua uwanja wa pili katika vita vya kimkoa dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa Boko Haram waliowauwa zaidi ya watu mia moja,wakiwemo wanajeshi 19 jumatano iliyopita kufuatia mapigano katika mji wa Fotokol wa Cameroon unaopakana na Nigeria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/

Mhariri Josephat Charo