1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger: Wanamgambo 280 wa Boko Haram Wauawa

John Juma APE, DPAE, RTRE
3 Januari 2019

Mapambano dhidi ya Boko Haram yashika kasi Nigeria na Niger. Jeshi linapambana ili kurejesha udhibiti wa mji muhimu wa kimkakati Baga, ambao kundi la Boko Haram liliuchukua wiki iliyopita.

Sahel Konflikt - Malische Armee
Picha: Getty Images/AFP/D. Benoit

Jeshi la Nigeria limesema helikopta yake imeanguka wakati mapambano yakishika kasi dhidi ya wanamgambo wa kundi la Boko Haram, kwa lengo la kudhibiti mji wa kimkakati Baga ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Kamanda wa jeshi la angani Ibikunle Daramola aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa ajali hiyo ya helikopta ilitokea Jumatano huku akiongeza kuwa mapigano yalikuwa yakifanyika eneo la Damasak, jimbo la Borno Kaskazini.

Vita vya kudhibiti mji wa Baga

Jeshi linapambana ili kurejesha udhibiti wa mji wa Baga, ambao kundi la Boko Haram liliuchukua wiki iliyopita. Mji huo ni kambi muhimu kwa majeshi ya kimataifa yanayopambana na wanamgambo.

Wakaazi wengi wa Baga wamekimbilia Maiduguri.

Mji wa Baga ulioko karibu na mpaka wa Chad, una silaha na vifaa vingine muhimu vya kijeshi ambavyo vinalengwa na wanamgambo.

Kando na mapigano yanayoendelea karibu na Baga, pamoja na ajali ya helikopta, maafisa 53 wa polisi hawajulikani waliko baada ya uvamizi uliofanywa na Boko Haram wiki iliyopita.

Wanamgambo 280 wa Boko Haram wauawa Niger

Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi katika baadhi ya nchi magharibi mwa Afrika.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Wakati hayo yakijiri, wizara ya Ulinzi nchini Niger imesema zaidi ya wanamgambo 280 wameuawa karibu na mpaka wa Nigeria kufuatia mashambulizi ambayo yamefanywa dhidi yao kwa siku kadhaa zilizopita.

Taarifa kutoka wizara hiyo imeeleza kuwa mashambulizi ya ardhini na angani dhidi ya kundi hilo yalianza Disemba 28, na kwamba zaidi ya wanamgambo wenye itikadi kali 200 wameuawa kufuatia mashambulizi ya angani.

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, Nigeria iliandaa mkutano wa dharura pamoja na nchi zilizoko karibu kuhusu kile ilichokitaja kuwa kuongezeka kwa mashambulizi kutoka kwa  wanamgambo wenye misimamo mikali kwa kutumia ndege zinazoendeshwa bila rubani.

Hofu ya mashambulizi ya Boko Haram?

Taarifa kutoka wizara ya ulinzi ya Niger imeeleza kuwa hakuna wanajeshi waliouawa wakati wa misako hiyo iliyofanyika mashariki mwa nchi hiyo.

Imeongeza kusema kuwa Nigeria imeathiriwa na mashambulizi kwenye kambi zao za kijeshi katika siku za hivi karibuni, na kwamba wanamgambo hao walikuwa wamejiimarisha.

Mwezi uliopita, waziri wa Ulinzi wa Niger alisema alihofia Boko Haram itaanzisha mashambulizi mapya kwanzia mwezi wa Januari wakati viwango vya maji katika mto Komadougou-Yobe huanza kupungua.

Mwandishi: John Juma/APE, DPAE, RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW