1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger yaruhusu chanjo ya malaria kwa watoto

Saleh Mwanamilongo
29 Aprili 2022

Serikali ya Niger imeidhinisha chanjo ya malaria itolewe kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ili kupambana na ugonjwa huo ambao uliuwa zaidi ya watu 4,000 nchini humo mwaka jana.

WHO Malawi Malaria Impfstoff
Picha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Afya wa Niger, Illiassou Mainassara, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali imeruhusu matumizi ya chanjo ya RTS-S, dhidi ya malaria, kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka sita ambao kila mwaka huathirika pakubwa na ugonjwa huo.

Anasema katika miezi ijayo, chanjo itafika Niger na hatua zote zimechukuliwa ili kufanikisha mpango huo. Taarifa ya baraza la mawaziri ilisema Niger ni mojawapo ya nchi zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya kampeni ya kupambana na malaria.

Tarehe 9 Oktoba mwaka wa 2021, WHO ilipendekeza chanjo hiyo aina ya RTS-S ya kampuni kubwa ya Uingereza, GSK, itolewe kwa wingi kwa watoto ili kupunguza kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa malaria. Tangu mwaka wa 2019, Ghana, Kenya na Malawi zilianza kutoa chanjo hiyo katika baadhi ya maeneo.

Kulingana na shirika la WHO, zaidi ya watoto milioni moja wamekwishapata chanjo hiyo katika nchi hizo, ikionyesha kupunguza kwa kiasi kikubwa visa vikali vya malaria.

Soma pia→WHO yaidhinisha chanjo ya kwanza dhidi ya Malaria


Chanjo ya malaria inaufanisi ?

Afrika bado kitovu cha malariaPicha: Brian ONGORO/AFP

Mkuu wa shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameitaja hatua hiyo kama "mafanikio ya kisayansi" ambayo huenda yakayabadilisha na kuyafanya kuwa mazuri, maisha ya mamilioni ya watu.

Waziri Mainassara anasema nchini Niger, idhini ya kuleta chanjo hiyo tayari imetolewa kwa washirika ikiwa ni pamoja na mashirika ya WHO na UNICEF. Mwaka jana watu 4,170 nchini Niger walikufa kutokana na malaria, na kuorodhesha visa milioni nne katika kipindi hicho. Djermakoye Hadiza Jackou, mratibu wa kitengo cha kitaifa cha  kupambana na malaria, alisema asilimia 50 ya visa na karibu asilimia 60 ya vifo nchini humo vinahusu watoto chini ya miaka mitano.

Anasema mchanganyiko wa chanjo hiyo na njia zingine za kuzuia, haswa vyandarua vilivyowekwa dawa, vitawezesha kupunguza angalau asilimia 75 ya visa vya malaria kwa watoto.

Soma pia→Watafiti wagundua aina sugu ya malaria barani Afrika

Fedha zimetengwa kusaidia juhudi hizi 

Kwa mujibu wa WHO zaidi ya dola milioni 155 zimepatikana kutoka kwa Gavi, ambao ni muungano wa chanjo duniani ili kusaidia kuanzishwa, ununuzi na utoaji wa chanjo ya malaria kwa nchi zinazostahiki zilizoko Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. 

Takriban asilimia 90 ya visa vya malaria duniani vimerekodiwa barani Afrika, ambapo watoto 260,000 hufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW